WABIA WA MAENDELEO WAOMBWA KUENDELEA KUCHANGIA MIRADI YA NISHATI VIJIJINI

Monday, November 30, 2020|Number of views (2726)|Categories: News, Events
WABIA WA MAENDELEO WAOMBWA KUENDELEA KUCHANGIA MIRADI YA NISHATI VIJIJINI
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Hassan Kimanta amewataka Wabia wa Maendeleo kuendelea kuchangia Mfuko wa Nishati Vijijini (REF) ili kuwezesha usambazaji wa nishati vijijini kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa maisha ya wananchi wa vijijini.

Akifungua Mkutano wa Pili wa Mwaka kati ya Wabia wa Maendeleo katika sekta ya nishati na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika hoteli ya Kudu iliyopo Wilaya ya Karatu Mkoa wa Arusha, Mhe. Kimanta alisema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) hauna budi kuweka mifumo madhubuti ya kusimamia fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na Wabia wa Maendeleo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kusambaza nishati vijijini.

“Nawasihi mtumie fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa kuzingatia muda ili miradi iweze kukamilika na kuwanufaisha wananchi.

Mhe. Kimanta alisema kuwa kazi nzuri ya REA katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini imesaidia kujenga ushawishi na imani kwa Serikali na hasa kwa Wabia wa Maendeleo kuendelea kutoa rasilimali fedha katika Mfuko wa Nishati Vijijini (REF) kwa ajili ya usambazaji wa nishati vijijini.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said alisisitizia usimamizi mzuri wa fedha zinazotolewa na Wabia wa Maendeleo utawezesha kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara ifikapo Juni 2021 na vitongoji vyote ifikapo Mwaka 2025.
“Sisi kama Wizara ya Nishati tunaridhishwa na usimamizi wa miradi hii ya REA, na sasa hivi tumefikia asilimia 78 ya upatikanaji wa umeme vijijini na takribani vijiji 9,800 tayari vimepatiwa umeme na asilimia 20 iliyobaki tunatarajia ndani ya mwaka mmoja tuikamilishe na baada ya hapo tunaanza kwenda kitongoji kwa kitongoji. Ni kazi kubwa ambayo inahitaji ushirikiano wa sekta na taasisi mbalimbali” alisema Mhandisi Said.

Pia Katibu Mkuu alitoa rai kwa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme na kuitunza kwa kuepuka uharibifu, kama vile kuchoma moto nguzo na kwamba kunapotokea uharibifu Serikali inalazimka kutumia fedha nyingi kufanya matengenezo ya miundombinu hiyo.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wabia wa Maendeleo wamewezesha kusambaza nishati, hususani ya umeme katika vijiji 9,884 ambavyo ni sawa na asilimia 80.5 ya vijiji vyote 12,268 vya Tanzania Bara.

“Wakala upo katika hatua za mwisho za kuwapata wakandarasi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye vijiji vilivyobaki ambavyo ni takriban vijiji 2,300 mradi ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka 2021” alisema.

Aidha, Wakili Kalolo alisema kati ya vitongoji 64,395 vilivyopo, jumla ya vitongoji 28,000 ambavyo ni sawa na asilimia 43.5 tayari vimepatiwa huduma ya umeme.
Wakili Kalolo aliwashukuru Wabia wa Maendeleo kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini na kuwahakikishia kuwa wataendelea kusimamia fedha zinazotolewa ili ziweze kuleta tija na ufanisi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga alisema kuwa Serikali kwa kushirikana na Wabia wa Maendeleo imefanya uwekezaji mkubwa katika miradi ya kusambaza nishati vijijini ambapo zaidi ya shilingi Trilioni tatu zimetumika.

“Tumeshirikiana na Wabia wa Maendeleo hivyo madhumuni ya Mkutano huu ambao unafanyika mara mbili kwa mwaka ni kuona fedha wanazotoa zimetumikaje na tumefanikiwa kufanya nini kulingana na mpango kazi na changamoto zipi ambazo tumekabiliana nazo katika kutekeleza miradi na tunazijadili kwa pamoja na kutafuta ufumbuzi kwa pamoja” alisema Mhandisi Maganga.

Akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya Wabia wa Maendeleo, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Mhandisi Francis Songela alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini. “Umeme ni maendeleo kwa hiyo tunaamini kwa kushirikiana na Serikali azma ya kufikisha umeme katika vijiji vyote itafikiwa,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la PSSSF, Ghorofa ya 7
Barabara ya Makole
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz

Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507

Please login or register to post comments.

«December 2021»
MonTueWedThuFriSatSun
293012345
6789101112
13141516171819
20212223242526
272829303112
3456789