UTEKELEZAJI WA MRADI KABAMBE WA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI AWAMU YA TATU (TURNKEY III) WAANZA

Thursday, February 9, 2017|Number of views (20273)|Categories: Announcements, Press Releases

Documents to download

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeanza utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu wa kusambaza nishati vijijini utakaojumuisha vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia mwaka huu wa fedha 2016/17 hadi 2020/21. Kati ya vijiji hivyo, vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa gridi na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi (off-grid).

Utekelezaji wa Mradi huu unajumuisha vipengele-mradi (project components) vitatu:

1. Densification - kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme (underline distribution trasformers) katika maeneo yenye miundombinu ili kufikisha umeme kwenye vitongoji ambavyo havijafikiwa na umeme;

2. Grid extension - kinacholenga kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikiwa kabisa na miundombinu ya umeme wa gridi; na

3. Off-grid Renewable - Uzalishaji na usambazaji wa nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya umeme wa gridi (off-grid) na kwenye visiwa.

Utekelezaji wa vipengele-mradi katika Mradi huu umeanza na upo katika hatua mbalimbali kama ilivyoainishwa hapa chini.

Kipengele-mradi cha Densification

Utekelezaji wake tayari umeanza kufuatia Mikataba iliyosainiwa Mwezi Desemba, 2016 katika mikoa sita ya Arusha, Iringa, Mara, Mbeya, Pwani, na Tanga kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 27 kutoka Serikali ya Tanzania na Norway, hivyo kuwezesha vijiji 305 kusambaziwa umeme.

Kipengele-mradi cha Grid Extension

• Kusambaza umeme kwenye vijiji 3,559 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara unaokadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 733.98 kutoka Serikali ya Tanzania, Norway, Sweden na Benki ya Dunia. Mradi utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 24 kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2017/18. Taratibu za ununuzi zinaendelea na wakandarasi wataanza kazi mwezi Machi 2017. Hadi sasa jumla ya vijiji 4,395 kati ya vijiji 12,268 ambayo ni sawa asilimia 36 vimeunganishwa na huduma ya umeme. Baada ya kukamilika kwa mradi huu, jumla ya vijiji 7,934 sawa na asilimia 65 vitakuwa vimefikiwa na umeme. Vijiji 4,334 vinavyosalia vitapelekewa umeme kuanzia mwaka wa fedha 2018/19 hadi 2020/21 kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

• Kusambaza umeme kwenye vijiji 121 katika maeneo yanayopitiwa na umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 kutoka katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga kwa gharama ya dola za Marekani milioni 30 kwa ufadhili wa Serikali za Norway na Sweden. Taratibu za ununuzi wa wakandarasi zinakamilishwa na utekelezaji utaanza mwezi Machi 2017.

Kipengele-Miradi cha Umeme wa Nje ya Gridi (Off-grid Renewable)

Miradi hii inayotekelezwa na sekta binafsi inahusisha kuendeleza na kusambaza nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi pamoja na kwenye Visiwa vilivyopo kwenye maziwa na katika Bahari ya Hindi. Jumla ya Dola za Marekani milioni 84 zimetengwa kwa ajili ya mradi huu ; kati ya hizo Dola za Marekani milioni 42 ni kutoka Serikali ya Uingereza na Dola za Marekani milioni 42 kutoka Benki ya Dunia. Wakala ulitangaza awamu ya kwanza ya mradi huu tarehe 23 Septemba, 2016 (1st Call for Proposals) kwa ajili ya kushindanisha waendelezaji binafsi na wajasiriamali wa nishati jadidifu kwenye maeneo ya nje ya gridi (off-grid mini grids). Awamu ya pili itatangazwa mwezi Aprili 2017, matangazo haya yatakuwa yanatolewa kwa awamu kila baada miezi sita. Wajasiriamali wa nishati jadidifu wanahamasishwa kushiriki katika utekelezaji wa mradi huu.

Hitimisho

Wakala unaishukuru Serikali kwa kuweka msisitizo kwenye miradi ya usambazaji wa nishati bora vijijini pamoja na kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara ifikapo Mwaka 2021; na kuongeza idadi ya vijiji vilivyofikiwa na huduma ya umeme hadi asilimia 85 mwaka 2025 na asilimia 100 Mwaka 2030.


Imetolewa na:

Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mawasiliano Towers, Ghorofa ya 2
Barabara ya Sam Nujoma
S. L. P 7990
Dar es Salaam, Tanzania

Barua Pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 22 2412001, +255 22 2412002, +255 22 2412003
Nukushi: +255 22 2412007


Documents to download

«May 2022»
MonTueWedThuFriSatSun
2526272829301
2345678
9101112131415
16171819202122
23242526272829
303112345