Mkurugenzi wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Francis Songela amesema Serikali kupitia REA imetoa kipaumbele kwenye kuongeza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na kuongeza kuwa Wananchi wanapaswa kuchangamkia teknolojia mbalimbali kwa kuwa suala hilo lipo kwa ajili ya kulinda afya za Watu, kuboresha maisha yao hususan kwa Wananchi wa vijijini.
Mhandisi Songela ameyasema hayo hivi karibu wakati wa ziara yake kwenye maonesho ya kibiashara ya kimataifa ya Saba Saba na kuongeza kuwa REA itaendelea kutoa elimu na hamasa ya matumizi ya teknolojia mbalimbali ili kuhakikisha Wananchi wengi hususan wa vijijini wanaongeza matumizi ya majiko bora yanayotumia mkaa salama, gesi na Umeme kwa kiwango kidogo ili kulinda afya na mazingira yao.
Mhandisi Songela amesema, maonesho ya Saba Saba ni uwanja wa kutoa elimu pamoja na hamasa kwa Wananchi wengi wanaopata nafasi ya kutembelea na kusisitiza, REA itaendelea kuwashirikisha Wadau wengi ambao ni wagunduzi na waendelezaji wa teknolojia hizo ili kuhakikisha Watanzania wengi wanahamasika na kuanza kutumia teknojia hizo.
“Kwenye maonesho haya, tumeleta Wadau mbalimbali ambao tunashirikiana nao katika kusambaza teknolojia mbalimbali, kuna makampuni mbalimbali ambayo yanatengeza majiko bora ya kupikia, ambayo yanatumia umeme kidogo, hiyo ni fursa pia kwa Sekta Binafsi kuwekeza kwenye nishati ya kupikia”. Amesisitiza Mhandisi Songela.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi, Mhandisi, Jones Olotu ametoa wito kwa Wananchi kuchangamkia fursa ya kuomba Mkopo wa Ujenzi na Uendeshaji Vituo Vidogo vya Mafuta Vijijini (Petroli na Dizeli) na kuongeza kuwa fursa ipo wazi na kusema mkopo huo ni wa riba nafuu ya asilimia tano (5) tu.
“Mwananchi, atakopeshwa fedha shilingi milioni 70, atakwenda kujenga kituo kidogo cha kuuza mafuta (Petroli au Dizeli), lakini pia Mkopaji atapewa mtaji wa kuweka mafuta kwa ajili ya kuendesha biashara hiyo, natoa wito kwa Watu wote wenye sifa, wachangamkie fursa hii. Mwisho wa kutuma maombi ya mkopo huo ni Tarehe 25 Agosti, 2023.” Alisisitiza Mhandisi, Olotu.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la PSSSF, Ghorofa ya 7
Barabara ya Makole
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507