DC BUHIGWE NA VIONGOZI REA WAJADILI MIRADI YA UMEME VIJIJINI
Na Veronica Simba - Kigoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy, wamemtembelea Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina na kujadiliana kuhusu utekelezwaji miradi ya umeme vijijini, wilayani humo.
Viongozi hao wamejadili kuhusu ufanisi, changamoto za miradi na namna ya kuzitatua kwa lengo la kufanikisha azma ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wote waishio vijijini wanafikishiwa nishati ya umeme awamu kwa awamu.
Kikao hicho kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, Desemba 22, 2021 kiliwashirikisha pia wataalam kutoka REA, TANESCO pamoja na Mkandarasi Kampuni ya M/s CCCE Etern Consortium ya nchini China, inayotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza wilayani humo.
Akiwasilisha taarifa mbele ya Mkuu wa Wilaya, Mwakilishi wa Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Evance Kabingo alieleza kuwa Wakala hiyo imeendelea kutekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani humo kwa ufanisi ambapo kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, jumla ya vijiji 22 vimepelekewa umeme, mashine umba 70 zimefungwa na wateja wa awali 2,496 wameunganishiwa umeme.
Akizungumzia kuhusu wananchi wote kufikiwa na huduma ya umeme, Mkurugenzi Mkuu alisema azma hiyo ya Serikali itatimizwa hatua kwa hatua kupitia miradi mbalimbali hivyo hakuna haja kwa mtu yeyote kuwa na hofu kuwa hatofikiwa.
Akieleza zaidi, Mhandisi Saidy alifafanua kuwa hatua ya kwanza inayoendelea kutekelezwa ni kuhakikisha miundombinu ya umeme inafika katika kila kijiji na kuunga wateja wa awali, kisha miundombinu hiyo itatumika katika kusambaza umeme kwa wakazi wote wa eneo husika, awamu kwa awamu.
“Nafahamu kuwa wapo wanaodhani kuwa wamerukwa na kwamba hawatafikiwa na umeme baada ya kuona miundombinu imefika katika vijiji vyao lakini wao hawajaunganishiwa. Niwatoe hofu kuwa wote watafikiwa hatua kwa hatua kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa,” alifafanua.
Kuhusu changamoto katika utekelezaji wa miradi husika, Mwenyekiti wa Bodi alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa ni pamoja na baadhi ya wakazi wa maeneo tofauti kuharibu miundombinu kwa kuchoma moto nguzo, kuiba vifaa mbalimbali pamoja na mwitikio duni kwa baadhi ya wakazi wa maeneo ambayo yamefikishiwa huduma ya umeme.
Kufuatia changamoto hizo, Wakili Kalolo alimwomba Mkuu wa Wilaya kutumia mamlaka aliyonayo ili kuweka mbinu mbalimbali za uelimishaji na uhamasishaji jamii katika kutatua na/au kuziepusha zisitokee.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya, pamoja na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na REA katika kutekeleza Ilani ya Chama Tawala kwa kusambaza umeme vijijini ili kuwaletea wananchi maendeleo, aliahidi pia kufanyia kazi ushauri uliotolewa, hususan katika utunzaji wa miundombinu na uhamasishaji jamii kuchangamkia fursa ya umeme.
Hata hivyo, Kanali Ngayalina aliwatoa hofu Viongozi wa REA kuwa wananchi wa Buhigwe siku zote wamekuwa na hamasa kubwa katika kuchangamkia fursa ya umeme na kwa wale ambao wameshafikishiwa nishati hiyo, wamekuwa wakiitumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuboresha maisha yao.
Aidha, aliomba katika miradi inayoendelea, kipaumbele kilenge Taasisi mbalimbali za umma pamoja na miradi ya maendeleo vikiwemo viwanda vidogo vidogo vya kuchakata kahawa.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi na Ujumbe aliofuatana nao walimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kueleza nia ya ziara yao ambapo walipokelewa na kufanya mazungumzo na mwakilishi wake, Katibu Tawala wa Mkoa, Rashid Mchatta.
Vilevile, viongozi hao walifanya mazungumzo na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya nishati vijijini katika Mkoa wa Kigoma na kujadiliana kuhusu mafanikio, changamoto na namna ya kuzitatua ili kukamilisha miradi kwa ufanisi.
Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu wa REA wako katika ziara ya kazi mkoani Kigoma kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la PSSSF, Ghorofa ya 7
Barabara ya Makole
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507