Social Links Search User Login Menu
Tools
Close
Close
Mikataba ya Bilion 50.98 Yasainiwa
Frank A. Mugogo 82

Mikataba ya Bilion 50.98 Yasainiwa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amesema Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kunakuwa na unafuu katika upatikanaji wa bidhaa za Nishati Safi ya kupikia ili kumwezesha kila mwananchi kutumia nishati iliyo safi na salama. 

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 13 Septemba 2024 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya Kusaini mikataba ya ushirikiano ya utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia yenye thamani ya shilingi bilioni 50.98 kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Jeshi la Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Wasambazaji wa Gesi ya kupikia, hafla ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa jengo la REA.

 “Namshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yanayowezesha Sekta ya Nishati kuendeshwa kwa mafanikio ambayo yamepelekea leo hii tushuhudie hatua ikizidi kupigwa katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuokoa maisha ya watanzania na pia kuiwezesha Wizara ya Nishati kutatua changamoto zinazojitokeza lengo likiwa ni kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi," amesema Dkt. Biteko 

Akizungumzia usambazaji wa nishati vijijini ikiwemo umeme, Dkt. Biteko ameipongeza Bodi na Menejimenti ya REA kwa kusimamia ipasavyo miradi na kwa kuwahimiza wakandarasi kukamilisha kazi kwa wakati. 

"Nawapongeza sana Bodi ya REA; mnafanya kazi nzuri, nimekuwa nikiwaona mara kwa mara mkiwa vijijini mnahimiza Wakandarasi," alipongeza. 

Akizungumzia jengo la REA alilolizindua, Dkt.Biteko amesema litawawezesha watumishi kutoa huduma kwa wananchi na kuwapongeza REA kwa kujenga jengo hilo la kisasa lenye ghorofa tano kwa gharama ya shilingi bilioni 9.8 kwa miezi 18 badala ya shilingi bilioni 13 zilizopangwa awali. 

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa majengo ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake yanafungwa mfumo wa umeme jua ikiwa ni kuonesha kwa vitendo matumizi ya nishati safi yenye gharama nafuu. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe.Daniel Sillo amesema tukio hilo ni alama ya ushirikiano kati ya REA na Taasisi za Jeshi ambapo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, udhibiti wa rasilimali za misitu na kutengeneza fursa za ajira kupitia Nishati Safi ya Kupikia. 

Amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) kuwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 ziache matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia Nishati safi ya Kupikia ikwemo gesi asilia, umeme, bayogesi na makaa ya mawe yaliyoboreshwa.

Amesema kwa sasa nishati inayotumika kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu ni kuni kwa asilimia 98 ambapo Jeshi hilo lilianza kutekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanza kutumia nishati safi kupitia gesi asilia na mkaa mbadala hivyo kusainiwa kwa mkataba huo kutawezesha Jeshi la Magereza kutumia nishati safi ya kupikia kwenye magereza yake. 

Amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani itahakikisha fedha zilizotengwa pamoja vifaa kwenye programu hiyo zinasimamiwa ipasavyo ili lengo tarajiwa lifikiwe na hii ikienda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa Jeshi ili waweze kuisimamia na kutunza miundombinu itakayofungwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa pongezi kwa REA kwa kukamilisha jengo kubwa la kisasa ambalo linaifaharisha Dodoma na pia amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa sh.bilioni 214 kwa ajili ya shughuli za umeme mijini na vijijini ambapo mkoani Dodoma asilimia 92.2 ya vijiji vimefikiwa na umeme huku kazi hiyo usambazaji umeme ikiendelea. 

Pia amemshukuru Rais, kwa miradi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia uhamasishaji wa nishati hiyo na kueleza kuwa kasi ya kutumia nishati safi kwa wananchi inaongezeka. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akizindua mjadala wa kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia na kutilia mkazo wakati akizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kwamba Wizara ya Nishati ina wajibu wa kutekeleza agizo hilo na ndio maana taasisi yake ya REA imesaini mikataba husika 

 Amesema Mikataba iliyosainiwa inahusisha masuala mbalimbali ikiwemo kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia pamoja na usambazaji wa majiko na mitungi ya gesi ipatayo laki nne ambayo inatolewa kwa bei ya ruzuku kwa wananchi hasa maeneo ya vijijini. 

 Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy alisema kuwa, Wakala kuhamia kwenye jengo lake kumewezesha kuokoa shilingi milioni 650 zilizokuwa zikitumika kwa mwaka kulipia kodi ya pango ambazo sasa zinaelekezwa kwenye maendeleo ya huduma zinazotolewa na Wakala. 

Kuhusu mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia alisema kwa upande wa Jeshi la Magereza, mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 35.23 ambapo kati ya fedha hizo 75.5% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 26.57 zitatolewa na REA na 24.6% sawa na shilingi bilioni 8.66 zitatolewa na Jeshi hilo kwa mradi utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika Magereza 129 ya Tanzania Bara. 

Mkataba wa Magereza unahusisha masuala mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mifumo ya bayogesi (gesi vunde) 126, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG, usimikaji wa mfumo wa gesi asilia, usambazaji wa mitungi ya gesi (LPG) ya kilo 15 ikiwa na jiko la sahani mbili ipatayo 15,920 kwa watumishi wa Magereza na usambazaji wa tani 865 za mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kutoka STAMICO. 

Mhandisi saidy alisema kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 5.75 ambapo kati ya fedha hizo asilimia 76 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 4.37 itatolewa na REA na huku asilimia 24 sawa na shilingi bilioni 1.39 itatolewa na JKT. 

Alisema fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi katika Kambi 22 za JKT kwa muda wa miaka miwili itakayohusisha ujenzi wa mitambo 9 ya bayogesi, majiko 291 ya kutumia mkaa mbadala (makaa ya mawe na tungamotaka), ujenzi wa mifumo 180 ya kupikia inayotumia LPG na sufuria zake, ununuzi wa tani 110 za mkaa unaotokana na makaa ya mawe, ununuzi wa mashine 60 za kutengeneza mkaa mbadala na mafunzo kwa vijana wapatao 50,000. 

Wadau wengine waliosaini mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia ni kampuni zinazofanya biashara ya gesi ya mitungi ikiwemo Taifa Gas, Manjis, Oryx pamoja na Lake Oil ambapo wanasambaza mitungi ya gesi ya kupikia ipatayo 452,445 kwa bei ya ruzuku katika mikoa yote ya Tanzania Bara.


Imetolewa na:

Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma

Share

Print
«November 2024»
MonTueWedThuFriSatSun
28293031123
456
Zaidi ya Bilioni 11 Kusambaza Umeme Vitongojini Shinyanga

Zaidi ya Bilioni 11 Kusambaza Umeme Vitongojini Shinyanga

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 11.18 wa kusambaza umeme katika vitongoji 90 utakaonufaisha Kaya 2,970 Mkoani Shinyanga.

Read more
78
REA Kufunga Mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia Shule ya Ruhinda

REA Kufunga Mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia Shule ya Ruhinda


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeahidi kujenga mifumo ya nishati safi ya kupikia pamoja na jiko katika shule ya Sekondari ya mchanganyiko ya Ruhinda iliyopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera.

Read more
910
111213

Report of the Controller and Auditor General on Financial and Compliance Audit for the Financial Year Ended 30 June 2023 for the Rural Energy Agency (REA)

Report of the Controller and Auditor General on Financial and Compliance Audit for the Financial Year Ended 30 June 2023 for the Rural Energy Agency (REA).

Read more
14
Call for Proposals to Supply Clean Cook Stoves for Promotions on Call Basis

Call for Proposals to Supply Clean Cook Stoves for Promotions on Call Basis

The Rural Energy Agency invites applications from qualified suppliers to submit proposals detailing the types of clean cooking solutions intending to supply clean cooking solutions across the country at subsidized rates. The proposal should also outline the actual costs and distribution expenses for providing these services in rural areas.

Read more
151617
18192021222324
2526272829301
2345678

Archive

Contact Us

E-Mail
General Information:  info@rea.go.tz
Director General:  dg@rea.go.tz
Procurement (PMU):  pmu@rea.go.tz
Webmaster:  webmaster@rea.go.tz

Mailing Address

Director General
Rural Energy Agency - REA
REA Building
28 Medeli Street
P. O. Box 2153
Dodoma, Tanzania

Phone & Fax

Tel: +255 26 2323504, +255 26 2323506
+255 26 2323507
Fax: +255 26 2323507

Time Zone

Please note that we are based in Tanzania, Time zone (GMT+03:00). Although we may not be in office at times convenient for all international enquiries, we do monitor our e-mail outside normal office hours.

Back To Top