Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kukamilisha jengo kubwa la kisasa ambalo linaifaharisha Dodoma na pia amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa sh.bilioni 214 kwa ajili ya shughuli za umeme mijini na vijijini ambapo mkoani Dodoma asilimia 92.2 ya vijiji vimefikiwa na umeme huku kazi hiyo usambazaji umeme ikiendelea.
Ametoa pongezi hizo tarehe 13 Septemba 2024 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya Kusaini mikataba ya ushirikiano ya utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia yenye thamani ya shilingi bilioni 50.98 kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Jeshi la Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Wasambazaji wa Gesi ya kupikia, hafla ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa jengo la REA.
Mhe. Senyamule amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia uhamasishaji wa nishati hiyo na kueleza kuwa kasi ya kutumia nishati safi kwa wananchi inaongezeka.
"Mhe. Rais amewezesha maeneo yote ya kimkakati hapa Dodoma kupata umeme ikiwemo eneo la umwagiliaji, vyanzo vya maji na eneo la viwanda na hii imeongeza kasi ya ukuaji wa Jiji la Dodoma," amesema.
Amesema ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia imepokelewa vyema na wananchi wa Dodoma na tayari vikundi kadhaa vimeundwa hususan vya kina mama na wananchi wenye mahitaji maalum na wamepatiwa uwakala wa bidhaa za nishati safi ya kupikia ambayo ni fursa kwao katika kujiongezea kipato
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma