Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Nishati Vijijini, Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Gideon Kingu amefanya mkutano wa kwanza na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) leo tarehe 06 Oktoba 2023. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassam alimteua Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini tarehe 25 Septemba 2023.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan S. Saidy alimkaribisha Mwenyekiti na kufafanua Muundo na Majukumu ya Wakala kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Nishati Vijijini Na. 5 ya Mwaka 2005. Aidha, Mkurugenzi Mkuu alieleza mipango na miradi iliyotekelezwa na Wakala tangu kuanzishwa kwake Mwaka 2007; mipango na miradi inayoendelea kutekelezwa; pamoja na mikakati itakayowezesha Serikali kufikia malengo ya kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na huduma bora na za kisasa za nishati vijijini kufikia Mwaka 2025.
Mha. Hassan saidy alimweleza Mhe. Mwenyekiti kuwa, pamoja na miradi ya umeme vijijini inayopanua gridi ya Taifa, pia kuna miradi ya nishati jadidifu ambayo inatekelezwa katika maeneo ambayo ni mbali na gridi ya Taifa pamoja na maeneo ambayo hayafikiki kirahisi na miundombinu ya gridi ya Taifa ikiwa ni pamoja na maeneo ya visiwani.
Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mha. Jones Olotu alitoa maelezo kuwa, wakati Wakala unaanza kutekeleza majukumu yake Mwaka 2007, upatikanaji wa umeme vijijini ulikuwa umefikia asilimia 2 tu na jumla ya vijiji 506 kati ya vijiji 12,318 vya Tanzania Bara vilikuwa vimefikiwa na miundombinu ya umeme. Tathmini iliyofanyika Mwaka 2020 ilionesha kuwa, hadi kufikia mwaka huo hali ya upatikanaji wa umeme vijijini ilifikia asilimia 69.6. Kwa sasa Wakala unaandaa kazi ya kutathmini hali ya upatikanaji umeme nchini kufikia mwaka 2025.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mha. Emanuel Yesaya alieleza mipango na miradi ya Wakala ya kusambaza nishati safi ya kupikia ukiwemo mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya LPG 70,200 kwa ajili ya kuwapatia wananchi nishati safi na salama ya kupikia; maendeleo ya mradi wa kujenga na kuendeleza vituo vya mafuta ya petroli na dizeli vijijini; uwezeshaji katika kutengeneza majiko banifu (Improved Cook Stoves); pamoja na kuwawezesha waendelezaji binafsi wanaotengeneza mkaa mbadala (briquettes). Aidha, kusimamia utekelezaji wa miradi ya gridi ndogo za umeme (mini grids) inayotekelezwa na waendelezaji miradi waliopata ruzuku mbalimbali kutoka kwa Wakala.
Mwenyekiti wa Bodi, Mhe. Balozi Meja Jenerali Mtaafu Jacob Gideon Kingu ameipongeza Menejimenti ya Wakala kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa weledi. Mwenyekiti ametoa rai kwamba, kama wataalamu tuhakikishe tunakamilisha utekelezaji wa majukumu na miradi kwa wakati. Amesisitiza kuwa, Wakala uhakikishe kuwa mikataba isimamiwe vizuri, manunuzi yafanyike kwa kufuata sheria, na malipo ya huduma mbalimbali yafuate tararibu ili kuepukana na hoja za ukaguzi.
Mwenyekiti alieleza kuwa atahakikisha anasaidia juhudi za Wakala katika utekelezaji wa shughuli na kwamba, watakapotangazwa wajumbe wa Bodi, watafanya kazi kwa pamoja na Menejimenti katika kufikia malengo ya Taifa kwamba, kila Kijiji na kila kitongoji kinafikiwa na huduma ya umeme.