Ubalozi wa Norway nchini umeandaa semina ya siku moja iliyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam tarehe 20 Septemba, 2016 kwa ajili kuelezea fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati nchini. Semina hiyo ilihudhuriwa na washiriki kutoka makampuni 14 kutoka Norway na wadau wengine mbalimbali.
Akifungua semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk. Juliana Pallangyo alisema ni fursa nzuri kwa washiriki kujifunza na kubadilishana uzoefu. Naibu Katibu Mkuu aliwahimiza wadau kutoka nchini Tanzania kushirikiana na wenzao wa Norway ambao wana uzoefu wa miaka mingi katika sekta ya nishati.
Akizungumza katika semina hiyo, Balozi wa Norway nchini, Hanne-Marie Kaarstad alisema kuwa ushirikiano wa Norway na Tanzania ni wa muda mrefu na umekuwa wa mafanikio ambapo shughuli mbalimbali za maendeleo zimetekelezwa kutokana na ushirikiano huo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga aliwahimiza waendelezaji wa miradi ya nishati kuchangamkia fursa hiyo na kueleza kuwa zipo fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya nishati ambazo zikitumiwa vizuri zitawezesha upatikanaji wa nishati hiyo vijijini.
Imeandaliwa na:
Jaina D. Msuya
Afisa Habari na Elimu kwa Umma
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mawasiliano Towers, Ghorofa ya 2
Barabara ya Sam Nujoma
S. L. P 7990
Dar es Salaam, Tanzania
Barua Pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 22 2412001, +255 22 2412002, +255 22 2412003
Nukushi: +255 22 2412007