TAARIFA YA KUANZA KWA UTEKELEZAJI WA MPANGO KABAMBE WA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI AWAMU YA TATU (TURNKEY III)
1. Utangulizi
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni Taasisi ya Serikali ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 8 ya Mwaka 2005 chini ya Wizara ya Nishati na Madini. Wakala unaratibu shughuli za Mfuko wa Nishati Vijijini (Rural Energy Fund – REF) chini ya usimamizi wa Bodi ya Nishati Vijijini (Rural Energy Board – REB). Oktoba 2007, Wakala ulianza kutekeleza majukumu yake rasmi kama yalivyoainishwa na Sheria ya Nishati Vijijini. Majukumu ya Wakala na Mfuko wa Nishati Vijijini ni kuwezesha upatikanaji na kuhamasisha matumizi ya nishati bora vijijini kwa:-
a) Kuibua na kuhamasisha miradi ya nishati vijijini;
b) Kuainisha na kutathmini miradi ya nishati inayostahili kupewa ruzuku kutoka Mfuko wa Nishati Vijijini;
c) Kufanya kazi na waendelezaji na kujenga uwezo wao katika kupanga na kutekeleza miradi ya nishati vijijini;
d) Kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu sera ya maendeleo ya nishati vijijini;
e) Kuwekeza katika miradi hamasishi ya nishati;
f) Kuibua, kutangaza na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini;
g) Kuhamasisha matumizi ya nishati bora katika shughuli za uzalishaji, kilimo, viwanda vidogo vidogo na vya kati, na biashara ili kukuza uchumi vijijini; na
h) Kuwezesha upatikanaji na matumizi ya nishati bora kwa ajili ya huduma za kijamii vijijini kama vile afya, elimu, maji na mawasiliano.
2. Kuanza kwa Utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (Turnkey III)
Serikali kupitia REA, imeanza utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu wa kusambaza nishati vijijini utakaojumuisha vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia mwaka huu wa fedha 2016/17. Kati ya vijiji hivyo, vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa gridi na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi (off-grid) kutokana na nishati jadidifu kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuvipelekea umeme kwa gharama nafuu kwa sasa. Hadi kufikia sasa jumla ya vijiji 4,395 kati ya vijiji 12,268 ambayo ni sawa asilimia 36 vimeunganishwa na huduma ya umeme.
Usambazaji wa umeme wa gridi ya taifa utahusisha:
a. kufikisha umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme wa gridi (gridi extension);
b. kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme (underline trasformers) katika maeneo yenye miundombinu ili kufikisha umeme kwenye vitongoji ambavyo havikufikishiwa umeme kwenye mradi wa Turnkey II (Densification) utakaotekelezwa kama sehemu ya Turnkey III; na
c. miradi ya uzalishaj na usambazaji wa nishati jadidifu (Off-grid) kwenye visiwa na maeneo ya vijijini yaliyo mbali na gridi itakayotekelezwa na sekta binafsi kwa ruzuku kutoka Mfuko wa Nishati Vijijini.
Inakadiriwa kuwa miradi ya kusambaza umeme wa gridi itagharimu takribani Shilingi Bilioni 7,000. Kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi Bilioni 4,000 ni kwa ajili ya kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikishiwa umeme katika mikoa na wilaya zote; na kiasi cha Shilingi Bilioni 3,000 kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye maeneo ambayo yameshafikiwa na miundombinu ya umeme lakini baadhi ya vitongoji na taasisi bado havijafikiwa na umeme. Gharama halisi zitabainishwa baada ya zabuni kupokelewa na kuchambuliwa. Fedha hizi zitatoka kwenye Bajeti ya Maendeleo ya Serikali kila Mwaka; tozo kwenye petroli na mafuta ya taa, tozo ya umeme na michango ya Washirika wa Maendeleo.
Utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu kwa vijiji 176 vilivyo mbali na gridi utaanza katika Mwaka wa Fedha 2016/17 na itatekelezwa na sekta binafisi kwa ruzuku kutoka Serikali kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo.
Miradi yote chini ya Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu itatekelezwa na wakandarasi binafsi kwa utaratibu wa Turnkey kwa usimamizi wa pamoja kati ya REA, TANESCO na Wakala wa Amana (Trust Agent).
3. Hitimisho
Hadi mwishoni mwa mwezi Juni 2016 miradi kabambe ya umeme vijijini Awamu ya Kwanza na Awamu ya Pili inayoendelea kukamilishwa, jumla ya vijiji 4,395 vilikuwa vimeunganishwa na huduma ya umeme sawa na 36% ya vijiji vyote 12,268 vya Tanzania Bara. Lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara ifikapo Mwaka 2021; na kuongeza idadi ya wanachi waopata huduma ya umeme hadi asilimia 85 mwaka 2025 na asilimia 100 Mwaka 2030.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Barabara ya Sam Nujoma, 14414
S. L. P 7990
Dar es Salaam.
Simu +255 22 2412001/2/3
Barua pepe: info@rea.go.tz