Serikali imesema ipo tayari kushirikiana na Ujerumani katika kuzalisha umeme
vijijini kwa kutumia nishati mbadala hususan upepo na jua. Hayo yalisemwa na
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Prof. Sospeter Muhongo alipokutana na Ujumbe
wa Wabunge kutoka Ujerumani.
Ujumbe wa Wabunge hao uliongozwa na Mhe. Josef Goeppel ambaye aliongozana na
Mhe. Dorothea Steiner, Mhe. Marco Brulow, Mhe. Sabine Stuber pamoja na balozi wa
Ujerumani nchini Mhe. Klaus-Peter Brandes.
Wabunge hao walimtembelea Waziri Prof. Muhongo ofisini kwake kwa lengo la
kujadili naye namna Ujerumani inavyoweza kushirikiana na Tanzania katika
kuwezesha wananchi wengi kupata huduma za umeme hususan kwa waishio maeneo ya
vijijini kwa kutumia vyanzo vya nishati mbadala.
Mhe. Prof. Muhongo alieleza Ujumbe huo kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana
na Serikali ya Ujerumani katika sekta ya nishati hususan nishati mbadala, katika
jitihada zake za kuwapatia wananchi nishati hiyo. “Sisi tupo tayari kushirikiana
nanyi katika suala hili la uzalishaji umeme, kwani lengo letu ni kuwa na umeme
wa kutosha na wa uhakika” alisisitiza Prof. Muhongo.
Naye Mhe. Joseph Goeppel ambaye pia ni Kiongozi wa Ujumbe wa Wabunge hao
alisema amefurahishwa na namna Tanzania ilivyojipanga katika kuwawezesha
wananchi wengi kupata huduma ya umeme ambayo ni kichocheo cha maendeleo.
Aliahidi kupeleka ujumbe huo katika bunge la Ujerumani ili kuanza rasmi
ushirikiano baina ya serikali hiyo na serikali ya Tanzania katika uzalishaji
umeme kwa kutumia nishati mbadala.
Mhe. Goeppel alimuomba Waziri Muhongo kuwa ushirikiano huo uanze mapema mwezi
Januari baada ya kukamilisha taratibu zote za kiofisi zinazohusu ushirikiano wa
kimataifa. Prof. Muhongo alikubali ushauri huo na kusema Serikali ya Tanzania ipo
tayari kuanza ushirikiano huo mapema iwezekanavyo.
Imeandaliwa na:
Mohamed Saif
Afisa Habari
Wizara ya Nisahati na Madini
mohamed.saif@mem.go.tz