Wabia wa Maendeleo ambao wanafadhili miradi ya kusambaza nishati vijijini wamepongeza Wakala wa Nishati Vijijini kwa utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini ambayo inaleta tija kwa ustawi wa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Wabia hao ambaye ni Naibu Balozi wa Norway na Mkuu wa Idara ya Ushirikiano, Kjetil Schie wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Mwaka kati ya REA na Wabia wa Maendeleo ambao umefanyika tarehe 05 Aprili 2024 katika hoteli ya Tanga Beach Resort and Spar iliyopo katika Mkoa wa Tanga.
Schie alisema kuwa wanatambua jitihada za Serikali za kusambaza nishati vijijini ikiwa ni pamoja na nishati safi ya kupikia na miradi ya kusambaza umeme vijijini pamoja na tija iliyopatikana, hivyo wataendelea kushirikiana na REA katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Awali akifungua Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani alisema utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini umechangia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Tanga na aliwataka wananchi wa Mkoa huo kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ili waongeze kipato na kukuza ajira.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Gideon Kingu aliwashukuru Wabia wa Maendeleo kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini na kuwahakikishia kuwa wataendelea kusimamia fedha zinazotolewa ili ziweze kuleta tija na ufanisi.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
28 Mtaa wa Medeli
41104 Tambukareli
Dodoma