Wananchi wa Kata ya Mabogini iliyopo katika Wilaya ya Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro wameshukuru Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wabia wa Maendeleo wanaofadhili miradi ya kusambaza nishati vijijini kwa kufikishiwa huduma ya nsihati ya umeme katika vijiji na vitongoji vyao.
Akizungumza wakati wa ziara ya REA na Wabia wa Maendeleo kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu na Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili iliyofanyika tarehe 26 Mei 2022 katika Kitongoji cha Shabaha, Diwani wa Kata ya Mabogini, Mhe. Bibianna Massawe alisema kuwa wanashukuru Serikali, REA na wafadhili kwa kupelekewa huduma ya nishati ya umeme ambayo imechangia katika kuboresha na kuongeza thamani ya maisha kwa wakazi wa eneo hilo.
Mhe. Massawe alisema kuwa kata hiyo ina vijiji 8 na vitongoji 45 ambavyo vyote vimepelekewa huduma ya nishati ya umeme. “REA imetusaidia sana katika kata yetu, tulikuwa na wakati mgumu sana kama mnavyoona nyaya za umeme zimetapakaa kata nzima. Watu wamepata huduma, wamebadilisha maisha na thamani ya maisha imebadilika kwa sababu, kama mnavyoona hapa tuna karakana ambayo vijana wanaranda mbao na kutengeneza samani kwa ajili ya maofisi na majumbani, wanapata fedha kupitia huduma hii ya umeme. Kwa hiyo mimi niseme kwanza nashukuru sana kwa huduma hii kwa sababu imebadilisha maisha ya wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Shabaha, Athuman Issa Msangi, alieleza kuwa mazingira ya kuishi eneo hilo kabla ya kupelekewa huduma ya umeme yalikuwa magumu. “kwa kweli tunashukuru sana. Mwanzoni tulipohamia hapa tulikuwa tunatembea na vibatari pamoja na sola. Kwa kweli REA wametuokoa sana, wametupa mradi mzuri sana. Pamoja na kwamba bado watu wengi hawajaungwa na umeme katika nyumba zao, bado sio tatizo kubwa, tunaomba huo mradi uliobaki kidogo watujazilizie kama kilomita mbili”, alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sanya, Hans Mkindi alisema kuwa upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme umerahisisha shughuli nyingi na kuondoa adha kwa wanawake. “Mwaka 2014 wanawake walikuwa wanatembea kilomita tatu kufuata mashine ya kusaga na kukoboa mpunga lakini sasa hivi tuna viwanda vidogo vidogo kwa maana ya mashine za kukoboa mpunga na kusaga mahindi na wakina mama wanasaga hapa hapa, hawapaiti zile kero za zamani. Kwa hiyo tunashukuru REA imekuja kukomboa mwananchi wa hali ya chini sana. Sasa kila mwananchi anamudu gharama za kuunganisha umeme kwa Shilingi 27,000 tu, hata mwenye chumba kimoja ana umeme na vibaka wamepungua kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu ajira zimeongezeka na vijana wako bize katika shughuli zao”, alisema.
Awali Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa REA, Mhandisi Jones Olotu alisema kuwa vijiji na vitongoji vyote vya kata ya Mabogini vimepelekewa huduma ya nishati ya umeme. “Wakati tunaleta mradi huu hapa mahitaji ya wigo wa wateja wa awali yalikuwa ni 240, lakini kutokana na mahitaji kuwa makubwa tukaongeza wigo wa ziada ambao wateja walifika 940. Lakini mahiatji halisi mpaka sasa hivi ni wateja 1,846 na bado nyumba zinaongezeka”, alisema.
Aidha, ujumbe huo pia ulitembelea kijiji cha Kambi ya Nyuki kilichopo Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro ambako wananchi walishukuru kwa kupelekewa huduma ya umeme na kuomba nishati hiyo iendelee kusambazwa katika maeneo yote ya kijiji chao. “Tunashukuru kupata huduma ya umeme, tumeletewa mashine hapa karibu, hatuendi tena Bomang’ombe, lakini watu wengi bado hatujapata umeme, ni wachache tu wamepata, lakini wazee kama sisi tunashukuru kwa sababu tumepata mashine hapa karibu,” alisema Christina Lodo.
Mwanakijiji wa Kijiji cha Kambi ya Nyuki, Izack Gideon Urassa alisema, “kwetu sisi REA ni fursa kubwa sana kwa sababu imewezesha vijana kupata ajira kupitia umeme. Kwa sababu vijana wanachomelea wanapata kazi za kutengeneneza magirili na wanachomelea vitu mbalimbali, wanajipatia kipato na kubwa zaidi tunasaga mahindi hapa. Zamani ilikuwa pakikucha asubuhi mama anatembea kilomita saba kutoka hapa kwenda Bomang’ombe au Rundugai. Sasa hivi saa 12 jioni mama anaanza kupepeta mahindi yake kuyapeleka mashine hapa karibu kwa hiyo ni fursa kwetu ambayo tumeweza kuifurahia sana kwa eneo hili. Ila changamoto iliyopo ni kwamba eneo lililopata umeme ni eneo dogo sana. Kijiji cha Kambi ya Nyuki kina wakazi zaidi ya 1,000 lakini waliopata umeme ni nusu”, alisema Urassa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo alisema lengo la ziara ni kukagua utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini na kuona namna ambavyo wananchi wamenufaika na huduma ya nishati ya umeme. “Tunawashuku Wabia wa Maendeleo ambao ni Umoja wa Ulaya, Norway, Sweden, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika na wadau wengine wote ambao wamekuwa wakitusaidia kila tunapowapelekea mahitaji. Ombi langu kubwa kwa wananchi, ni vizuri tukaitunza hii miundombinu. Kuna maeneo ambayo tunapita tunakuta kifaa kimeng’olewa katika nguzo au kuwasha moto katika miundombinu. Tunaomba tushirikiane wote kuhakikisha kwamba miundombinu hii tunailinda kwa ajili ya kuendelea kupata huduma ya umeme”, alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Wabia wa Maendeleo, Meneja wa Miradi wa Umoja wa Ulaya, Mhandisi Francis Songela alisema wamefurahi kuona umeme umekuwa ni zaidi ya kuwasha taa kwa maana ya kwamba wananchi wameona umeme ni fursa kwa kujihusisha katika shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato kiuchumi. “Tumesikia wametaja biashara mbalimbali hicho ndio cha manufaa. Kingine tulichojifunza hapa ni mahitaji makubwa ya umeme na ni tofauti na maeneo mengine, idadi ya watu waliounganisha umeme ni kubwa sana. Inatupa faraja kwamba kweli umeme ni kipaumbele cha wananchi”, alisema.