Serikali na Wabia wa Maendeleo Katika Sekta ya Nishati (EDPG) wamechangia zaidi ya shilingi trilioni nne kwa ajili ya Miradi ya kusambaza nishati vijijini inayotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila amesema kuwa toka REA ianzishwe, Serikali imechangia jumla ya Shilingi Trilioni tatu wakati Wabia wa Maendeleo wamechangia Shilingi Trilioni moja kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini (REF).
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka kati ya REA na Wabia wa Maendeleo wanaofadhili Miradi ya kusambaza nishati vijijini uliofanyika tarehe 27 Mei 2022 katika hoteli ya Salinero iliyopo mkoani Kilimanjaro, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Rwebangila alisema kuwa fedha hizo zimetumika kupeleka miundombinu ya umeme katika ngazi ya vijiji. “Hatua ya kwanza ni kupeleka miundombinu ya umeme katika vijiji vyote na ifikapo Desemba mwaka huu tuwe tumegusa kila kijiji. Hii ilikuwa ni hatua ya kupeleka umeme katika vijiji na watu wengi wanalalamika kuwa hawajafikiwa na huduma ya umeme. Hawa wadau wa maendeleo wakati Serikali ikipeleka miundombinu wamekuwa wakitusaidia kujazia yale maeneo ambayo yameshafikiwa na miundombinu” alisema.
Mhandisi Rwebangila alisema kuwa kulinga na kiwango cha fedha za bajeti ambacho kinatolewa kila mwaka itachukua miaka kati ya 18 hadi 20 kukamilisha kupeleka umeme katika vitongoji vyote. Hivyo Wizara inapanga mikakati ambayo itapunguza huo muda wa kupeleka umeme katika vitongoji ufikie miaka mitano. “Tunafurahi kuwa tunapata changamoto kwa maendeleo tuliyoleta, wakati tunaanza wachache sana walihamasika na umeme, lakini leo kila mtu amehamasika.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy alisema kuwa, lengo la Mkutano huo ni kujadili Mpango Kazi wa Mwaka Pamoja na bajeti ya Wakala. “Tunatambua mchango wa Wabia wa Maendeleo ambao wanatoa fedha za kutekeleza Miradi ya kusambaza nishati vijijini kwa lengo la kuwapatia wananchi nishati bora. Nawashukuru na kuwapongeza Wabia wetu kwa msaada ambao wamekuwa wakitoa toka kuanzishwa kwa Wakala”.
Mhandisi Saidy alisema kuwa jitihada za Serikali na Wabia wa Maendeleo zimewezesha upatikanaji wa huduma za umeme vijijini kuongezeka kutoka asilimia mbili Mwaka 2007 wakati Wakala unaanzishwa hadi kufikia asilimia 70 Mwaka 2020.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo amewashukuru Wabia wa Maendeleo kwa mchango wao katika Miradi ya kusambaza nishati vijijini. “Nitumie fursa hii kuwashukuru Wabia wa Maendeleo kwa sababu wamekuwa wakichangia mpaka asilimia 25 ya bajeti ya Wakala wa Nishati Vijijini kwa ajili ya Miradi ya kusambaza nishati vijijini. Mkutano huu kwa kawaida unatusaidia kuwapeleka Wabia wa Maendeleo katika Miradi waliyofadhili kuweza kuona utekelezaji wa Miradi na tija ya Miradi hiyo kwa wananchi”, alisema.
Awali akifungua Mkutno huo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Steven Kigaigai aliipongeza REA kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya kusambaza miundombinu ya umeme vijijini. “Katika Mkoa wa Kilimanjaro, vijiji 11 tu ndiyo havina umeme, hivyo nawapongeza na kuwashukuru. Bado tunawahitaji REA kwa sababu ya mahitaji makubwa ya kuleta maendeleo ya nchi”, alisema.
Mwenyekiti wa EDPG, Bjorn Midthun aliipongeza REA na Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri ya kusambaza nishati vijijini ambayo aliitaja kuwa inalenga kutimiza malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yenye azma ya kuondoa umaskini na kuna umuhimu wa watu wa vijijini kupata umeme wa bei nafuu ili waweze kuutumia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na huduma za elimu, afya, maji pamoja na kutunza mazingira kwa ajili ya kuboresha ustawi wa maisha ya watu vijijini.
Midthun alisema Wabia wa Maendeleo wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini na kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo. Hata hivyo, alishauri REA kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania wafanye tathimini ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini kwa ajili ya kujua mafanikio na changamoto za utekelezaji wake na kuweka mikakati ya baadaye.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la PSSSF, Ghorofa ya 7
Barabara ya Makole
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507