Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la kisasa la Ofisi zake Jijini Dodoma.
Ametoa pongezi hizo baada ya kuzindua Jengo hilo Septemba 13, 2024 Jijini Dodoma katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa Serikali na wananchi wa maeneo ya jirani.
Dkt.Biteko amesema Jengo hilo litawawezesha watumishi kutoa huduma kwa wananchi na kuwapongeza REA kwa kujenga jengo hilo la kisasa lenye ghorofa tano kwa gharama ya shilingi bilioni 9.8 kwa miezi 18 badala ya shilingi bilioni 13 zilizopangwa awali.
Pamoja na pongezi hizo, Dkt. Biteko amewakumbusha kuhakikisha uwepo wa jengo hilo unakwenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa majengo ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake yanafungwa mfumo wa umeme jua ikiwa ni kuonesha kwa vitendo matumizi ya nishati safi yenye gharama nafuu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy alisema kuhamia katika jengo hilo kumeiwezesha REA kuokoa kiasi cha shilingi milioni 650 zilizokuwa zikitumika kwa mwaka kulipia kodi ya pango ambazo sasa zinaelekezwa kwenye maendeleo.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma