Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Bilioni 14 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Umeme kwenye vitongoji 135 Mkoani humo katika majimbo yote.
Ametoa shukrani hizo Septemba 18, 2024 alipotembelea kitongoji cha Bushweka kijiji cha Mulahya Kata ya Katerero, kuzungumza na wananchi kwa niaba ya wakazi wa Mkoa wa Kagera akiwa pia ameambatana na ujumbe wa Wakala Wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na CCC International Nigeria Engineering Ltd Ambaye Ndie Mkandarasi wa mradi huo.
Mhe. Fatma Mwassa amewasihi na kuwaasa wananchi wa Mkoa wa Kagera kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mkandarasi ili aweze kukamilisha utekelezaji wa mradi ndani ya wakati na kwa viwango vinavyokubalika.
Vilevile Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wakala kumsimamia Mkandarasi vema ili akamilishe mradi kwa wakati na kwa viwango kama mkataba unavyomtaka ili kwa haraka huduma za umeme ziweze kuwafikia wananchi.
Mhe. Fatma Mwassa amesema Mhe. Rais anaendelea kuboresha maisha ya wananchi wake kwa kasi ndio maana amemaliza kupeleka huduma za umeme kwenye vijiji vyote nchini na sasa anaelekeza nguvu kwenye vitongoji kwa kuhakikisha wanapata nishati safi.
Awali, Msimamizi wa miradi ya Wakala wa Nishati vijijini (REA) Kanda ya ziwa Mhandisi Ernest Makale amesema mradi huo kwenye vitongoji unadhihirisha na kubainisha nia ya serikali ya kuhakikisha kila kitongoji nchini kinakua na umeme ifikapo 2030.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma