MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI KITAIFA YALIYOFANYIKA KIJIJI CHA , BUTIAMA, MKOA WA MARA
Tarehe 5 Juni, kila mwaka Watanzania wanaungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Kitaifa maadhimisho haya yalifanyika katika Kijiji cha Butiama, Mkoani Mara ambako Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulishiriki.
Katika maadhimisho hayo, Wakala ulipata fursa ya kuonesha mpango wake wa kusambaza umeme vijijini katika Mkoa wa Mara na mikoa mingine pamoja na kupokea maoni na mahitaji ya wananchi wa Mkoa wa Mara ambao hawajafikiwa na huduma ya umeme.
Katika kuonesha uhalisia wa miradi ambayo inatekelezwa na Wakala, wakandarasi na waendelezaji wa miradi ya nishati vijijini walishiriki katika maadhimisho hayo kupitia banda la Wakala ambao ni pamoja na:
i. DERM Electric – Mkandarasi wa kusambaza umeme vijijini katika Mkoa wa Mara (Mradi Kabambe Awamu ya II);
ii. Angelique International Ltd – Mkandarasi wa kusambaza umeme vijijini katika Mkoa wa Mara (Mradi Kabambe Awamu ya III, kipengele cha Densification); na
iii. PowerGen Renewable Energy – Mradi wa umeme-jua (Solar Mini grid - LRTC 2014) katika eneo la Raranya, mkoani Mara.
Madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni kuhamasisha jamii kuelewa masuala yahusuyo mazingira na kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda mazingira. Kauli Mbiu iliyoongoza maadhimisho haya kitaifa ni “Hifadhi ya Mazingira: Muhimili kwa Tanzania ya viwanda”, lengo likiwa ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira wakati tunapokuza maendeleo ya viwanda nchini.
Wakati wa maadhmisho hayo, banda la Wakala wa Nishati Vijijini lilitembelewa na wageni mbalimbali ikiwa ni pamoja na mgeni rasmi wakati wa kilele cha maadhmisho hayo ambaye alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan. Pia wakazi wa kijiji cha Butiama, vitongoji mbalimbali na maeneo mengine ya Mkoa wa Mara walitembelea banda la Wakala wakiwa na shauku ya kujua utekelezwaji wa miradi mbalimbali.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mawasiliano Towers, Ghorofa ya 2
Barabara ya Sam Nujoma
S. L. P 7990
Dar es Salaam, Tanzania
Barua Pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 22 2412001, +255 22 2412002, +255 22 2412003
Nukushi: +255 22 2412007