Naibu Waziri Wizara ya Maji Nishati na Madini Zanzibar, Zawadi Nassor ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa hatua unazochukua, mikakati na mipango inayoendelea nayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi za Kupikia.
Ametoa pongezi hizo Agosti 24, 2024 baada ya kutembelea Banda la Wakala katika Maonesho ya Kizimkazi yanayofanyikia Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
"Tulichokishuhudia hapa na maelezo tuliyopata tumehamasika na tutakaa na pacha wetu kwa maana ya Wizara ya Nishati Bara ili tuone ni vipi nasisi tunaweza kuhamasisha wananchi wetu kutumia Nishati Safi ya Kupikia na kuachana na kuni," amesema Zawadi.
Alibainisha kuwa kufika kwake katika Banda la REA kumemuongezea uelewa wa uwepo wa baadhi ya bidhaa za Nishati Safi za Kupikia ambazo hajapata kuziona hapo kabla ambazo alisema kwa ufanisi wake ametamani ziwafikie wananchi wengi zaidi visiwani humo.
"Baadhi ya majiko hapa sikuwahi kuyaona hapo kabla, lakini kufika hapa nimejionea na nimeshuhudia namna yanavyofanya kazi, yanahamasisha; ni muhimu sasa nasi tukashirikiana na wadau na tukaongeza kasi ya kuhamasisha wananchi," alisema.
Alisema kwa upande wa Bara tayari mwamko wa matumizi ya bidhaa za Nishati Safi za Kupikia ni mkubwa ikilinganishwa na Zanzibar na alitoa wito kwa watengenezaji, wawekezaji, wauzaji na wasambazaji wa bidhaa hizo kuwekeza Zanzibar ili kusogeza huduma kwa wananchi.
"Tutashirikiana kwa karibu na Wizara ya Nishati Bara ili kuona namna bora ya kusogeza bidhaa hizi kwa wananchi sambamba na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwani wenzetu tayari wamepiga hatua," alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alimueleza Naibu Waziri huyo majukumu ya Wakala na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Wakala na wadau wengine ili kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa za Nishati Safi za Kupikia.
"Kwa sasa tunatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao ulizinduliwa Mwezi Mei mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambao umesisitiza kuwa kufikia 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia," alisema Mhandisi Advera.
Akizungumzia ushirikiano na mchango wa Serikali kupitia REA kwa wadau wa bidhaa za Nishati Safi za Kupikia Mhandisi Advera alisema REA inawawezesha kifedha wauzaji, watengenezaji na wasambazaji wa bidhaa za Nishati Safi za Kupikia kwa namna mbalimbali ikiwemo utoaji wa ruzuku kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anamudu gharama na pia kuhakikisha kila eneo linafikiwa na huduma.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma