Serikali Imetoa Shilingi Billioni 50 kwa Waendelezaji Wadogo Wadogo wa Miradi ya Nishati Jadidifu
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa takribani Shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya kuwawezesha waendelezaji wadogo wadogo kwenye miradi ya nishati jadidifu katika maeneo yaliyopo vijijini Tanzania Bara.
Nishati hizo ni pamoja na umeme unaozalishwa kutokana na vyanzo vya jua, upepo, maporomoko madogo ya maji pamoja na tungamo taka. Fedha hizi zimetolewa kufanikisha kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa taarifa za awali za mradi (upembuzi yakinifu), mpango biashara pamoja na taarifa za mazingira. Pia fedha zimetolewa kwa ajili ya kuunganisha wateja wakati wa utekelezaji wa mradi pamoja na kuwakopesha waendelezaji hao kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo.
Akifungua kikao cha pili kati ya Wizara ya Nishati, REA, TANESCO, EWURA na Waendelezaji hao kilichofanyika Septemba 19, 2019 katika ukumbi mdogo wa Bunge jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Merdad Kalemani (Mb) alisema Serikali inatambua mchango wa waendelezaji hao wa nishati ambao hadi sasa wamezalisha umeme wa takribani 17MW ambao umeingizwa katika gridi ya Taifa na mwingine kuwauzia moja kwa moja wananchi wa vijijini. Mh. Waziri alisema kuna dola za Marekani Milioni 54.5 kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji binafsi. Fedha hizi zimetengwa kwa Mwaka wa Fedha 2019/20. Aidha Dr. Kalemani alisisitiza kuwa, Serikali imeweka lengo la kuzalisha umeme wa 10,000MW ifikapo Mwaka 2025, hivyo anategemea waendelezaji binafsi wachangie katika uzalishaji huu ili kufikia lengo hilo.
Alisema kuwa waendelezaji miradi wote walioingia mikataba na REA ya kusambaza umeme katika vijiji 120, hadi sasa ni vijiji 82 kati ya hivyo vimefikiwa na huduma ya umeme na kuagiza vijiji vilivyobaki vikamilishwe ili kutimiza Mpango wa Serikali wa Kusambaza Umeme Vijijini (2016/17 – 2021) la kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote ifikapo Juni 2021.
Mh. Waziri aliwataka waendelezaji hao kujielekeza katika kutimiza lengo hilo la kuvipatia vijiji vyote umeme na kusisitiza ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na Serikali kwa ajili ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya umeme ili kuwawezesha wananchi kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha ustawi wa Maisha vijijini. Alisema kuwa hadi sasa kuna jumla ya waendelezaji wa miradi takribani 110 ambapo kati yao, waendelezaji 62 wamepatiwa ruzuku kwa ajili ya kuandaa taarifa za awali lakini ni waendelezaji 18 tu ambao wameanza kujenga na kusambaza miundombinu ya umeme katika maneo mbali mbali yaliyopo nje ya gridi ikiwa ni pamoja na maeneo ya visiwani Tanzania Bara.
Akiongea katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Nishati Mh. Subira Mgalu (Mb) aliwataka waendelezaji wa miradi ya nishati wawekeze zaidi na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme ili utumike katika uanzishwaji wa viwanda.
Awali akimkaribisha Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua alisema lengo la kikao hicho ni kujadili changamoto zinazowakabili waendelezaji wa miradi midogo ya nishati na vilevile kuwafahamisha fursa zilizopo.
Kwa upande wao waendelezaji hao walisema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa cheti cha ubora wa mazingira kutoka Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kuomba Serikali kurahisisha upatikanaji wake.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la LAPF, Ghorofa ya 7
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507