Waziri wa Nishati Akutana na Bodi na Wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini
Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Merdad Kalemani (Mb) ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuwahamasisha wananchi wa vijijini ambako miradi ya kusambaza umeme inatekelezwa kutumia umeme kwa ajili ya kujenga viwanda vya kusindika mali ghafi ambazo zinazalishwa vijijini.
Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo wakati akiongea na Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Menejimenti na Wafanyakazi wa REA katika kikao kilichofanyika Septemba 27, 2019 katika jengo la LAPF, jijini Dodoma na kusema ili Serikali iweze kujenga uchumi wa viwanda na kuwapeleka Watanzania katika uchumi wa kati ifikapo Mwaka 2025 inahitajika huduma ya umeme iwe imewafikia wananchi wengi wa vijijini na waitumie.Mh. Waziri aliagiza kuwa REA wahakikishe umeme unaokwenda vijijini unaakisi lengo la Serikali la kujenga uchumi wa viwanda, mali ghafi za viwanda zinatoka vijijini sasa mali ghafi hiyo ibaki huko huko na hatimae vijiji hivyo vibadilike viwe miji.
Ili kuweza kutimiza lengo hilo, Waziri Kalemani aliwaagiza REA kuhakikisha kuwa kufikia 30 Juni 2021 vijiji vyote vya Tanzania Bara viwe vimefikishiwa huduma ya umeme. Aliagiza kuwa kila mtumishi ahakikishe anasimamia ipasavyo kazi yake ili lengo tulilojiwekea liweze kutimia la kupeleka umeme vijijini kwa muda uliopangwa na kwa ufanisi. Mh. Waziri aliongeza kuwa kila mtumishi wa Wakala ajielekeze katika lengo hilo ili kufanikisha kujenga uchumi wa viwanda na kila mtumishi afanye kazi kwa kuzingatia mambo matatu, ambayo ni weledi, ubunifu na kwa kasi.
Aidha, Mh. Waziri amewaaagiza wasimamizi wa miradi ya kusambaza umeme vijijini kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha miundombinu inajengwa kwa kiwango kinachotakiwa na inakamilika kwa wakati uliopangwa. Pia Mh. Waziri amewataka REA kuanza mapema maandalizi ya utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ili ifikapo Januari 31, 2020 mradi huo uanze kutekelezwa.
Dkt. Kalemani ametaka taratibu za manunuzi zizingatiwe wakati wa kuwapata wakandarasi wa kutekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili na kuagiza kuwa hatavumilia kusikia migogoro ya aina yoyote.
Waziri alipongeza Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wa REA kwa kufanya kazi nzuri ambayo imechangia kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi wa vijijini.
Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Dkt. Andrew Komba alimuahidi Waziri kuwa Bodi itasimamia utekelezaji wa maagizo yote ili kukamilisha miradi kwa muda uliopangwa na kuongeza kuwa kasi hii itatumika pia katika kutekeleza Mradi wa REA III Mzunguko wa Pili, ili kuhakikisha kwamba itakapofika Juni 2021 vijiji vyote vya Tanzania Bara viwe vimepatiwa huduma ya umeme. Aidha, Dr. Komba alisema Wakala unakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha kutokana na mahitaji makubwa ya miradi ya umeme vijijini ikilinganishwa na upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la LAPF, Ghorofa ya 7
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507