UFAFANUZI KUHUSU HABARI ILIYOCHAPISHWA KATIKA GAZETI LA JAMHURI TOLEO NA. 295 LA TAREHE 23 – 29 MEI, 2017
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatoa ufafanuzi kuhusu habari iliyochapishwa katika gazeti la Jamhuri Toleo Na. 295 la tarehe 23 – 29 Mei, 2017 yenye kichwa cha habari “Waziri apiga dili” ununuzi wa zabuni ya wakandarasi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwamba ulizingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 (kama ilivyofanyiwa marekebisho Mwaka 2016) pamoja na kanuni zake. Wakala unakanusha uwepo wa upendeleo au ushawishi kutoka kwa viongozi wakishirikiana na wakandarasi walioomba zabuni hiyo.
Wakala unafafanua kwamba: Makampuni yaliyoshinda zabuni yalipatikana kwa kuzingatia Sheria na Taratibu za Ununuzi wa Umma na vigezo vilivyowekwa katika kabrasha la zabuni. Aidha, uchambuzi wa zabuni zilizowasilishwa na waombaji wa zabuni ulizingatia Sheria na Miongozo iliyotolewa katika kabrasha la zabuni.
Kuhusu tuhuma kuwa “kuna kampuni zilizopewa zabuni lakini zikiwa hazikusajiliwa katika Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB)” na “ kampuni ambazo hazikusajiliwa CRB lakini zimeshiriki na wabia ambao ni wa madaraja ya chini wasiostahili kupewa zabuni kubwa” ambapo zimetajwa kampuni za Guangdong Jianneng Electric Power Engineering na ubia wa Joe’s Electrical Ltd, AT & C Pty Ltd na L’S Solutions Ltd. Kampuni ya Guangdong Jianneng Electric Power Engineering (kampuni ya nje) iliwasilisha zabuni kwa ubia na kampuni ya Whitecity International Contractors Limited ambayo ilisajiliwa na CRB tarehe 03 Mei 2012 kama mkandarasi wa umeme Daraja la IV kwa Hati Na. 00625; Aidha, kampuni za Joe’s Electrical Ltd na AT & C Pty Ltd (kampuni za nje) ziliwasilisha zabuni kwa ubia na kampuni ya L’S Solutions Ltd ya Tanzania ambayo ilisajiliwa na CRB tarehe 04 Agosti 2009 kama mkandarasi wa umeme Daraja la VII kwa Hati Na. 0346. Kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011, Kifungu 51 (3) kampuni za nje zinaruhusiwa kushiriki katika zabuni ama peke yao au kwa ubia na kampuni za ndani au nje kabla ya kusajiliwa na CRB. Wakandarasi wanasajiliwa na CRD kwenye Daraja la I baada ya kupata barua ya tuzo kama wanakidhi vigezo. Kwa sasa Wakala wa Nishaji Vijijini umetoa barua za tuzo na kuagiza walete usajili toka CRB kabla ya kusainiwa kwa mkataba wa zabuni.
Kuhusu tuhuma kuwa “kampuni ambazo hazikusajiliwa CRB lakini zimeshirikiana na wabia ambao ni wa madaraja ya chini wasiostahili kupewa zabuni kubwa” ambapo zimetajwa kampuni za Radi Service Limited, Njarita Contractors Ltd na Aquila Electrical Contractors Limited (kampuni za ndani), kampuni hizi zimesajiliwa na CRB kwenye madaraja ya III kwa Radi Service Limited, daraja la V kwa Njarita Contractors Ltd na daraja la V kwa Aquila Electrical Contractors Limited. Kwa mujibu wa Sheria (Contractors Registration Act CAP 235 RE 2002) na ufafanuzi uliotolewa na CRB kwa Wakala wa Nishati Vijijini kwa barua yenye Kumb. Na. EI/0037/10/2009/35 ya tarehe 17 Mei 2017; hivyo ushiriki wa kampuni hizo katika zabuni hiyo ni halali. Wakandarasi wa ndani wanaruhusiwa kushiriki katika zabuni kwa ubia wakiwa na kibali cha CRB kushiriki kwenye zabuni husika. Ubia wao unasajiliwa kwenye Daraja la I na CRB baada ya kupata barua ya tuzo kwa ajili ya kutekeleza mradi katika zabuni husika. Tayari Wakala wa Nishati Vijijini umetoa barua ya tuzo na kuagiza wakamilishe taratibu za usajili toka CRB kabla ya kusainiwa kwa mkataba. Aidha, ubia wa kampuni za MF Electrical Engineering na GESAP Engineering Group Limited kupatiwa zabuni walizoshinda ni halali kwa kuwa kampuni ya MF Electrical Engineering ambayo ilisajiliwa na CRB tarehe 03 Desemba 2015 kama mkandarasi wa umeme Daraja la I (specialized contractor – Electric Powerlines and Systems) kwa Hati Na. 0367 na GESAP Engineering Group Limited ambayo ilisajiliwa na CRB tarehe 30 Juni 2015 kama mkandarasi wa umeme Daraja la I kwa Hati Na. 00768.
Kampuni ya Al- Hatimy Developers Limited ina usajili wa CRB kama mkandarasi wa umeme Daraja la I kwa Hati Na. 0566 iliyotolewa tarehe 11 Septemba 2012 ambapo NIPO Group Limited iliwasilisha zabuni kwa ubia wa Nipo Africa Limited yenye usajili wa CRB kama mkandarasi wa umeme Daraja la V kwa Hati Na. 0409 iliyotolewa tarehe 19 Desemba 2014 na kampuni ya Kellogg Construction Limited yenye usajili wa CRB kama mkandarasi wa umeme Daraja la V kwa Hati Na. 00751 iliyotolewa tarehe 19 Februari 2014. Kwa sasa Wakala wa Nishati Vijijini umetoa barua za tuzo kwa kampuni hizo, ambapo ubia wa NIPO Group Limited umeagizwa kuwasilisha usajili toka CRB kabla ya kusainiwa kwa mkataba; na kwa kampuni ya Al – Hatimy Developers Limited na kampuni nyingine zote za ndani zilizopewa barua za tuzo uhakiki wa madaraja yao kwa CRB unafanyika kabla ya kusaini mikataba.
Mchakato wa kuthibitisha uhalali wa wakandarasi na nyaraka walizowasilisha unaendelea kufanyiwa kazi na Wakala kabla ya kusaini mikataba. Ikumbukwe kuwa kilichofanyika ni kutoa barua za tuzo kwa wakandarasi. Wakandarasi watasaini mikataba baada ya kukamilika kwa hatua zinazofuata, baada ya kutolewa kwa barua za tuzo. Dosari itakayoonekana kwenye hatua yoyote ya mchakato kwa mkandarasi yeyote itasababisha mkandarasi kunyang’anywa mradi alioshinda.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Barabara ya Sam Nujoma, 14414
S. L. P 7990
Dar es Salaam.
Simu +255 22 2412001/2/3
Barua pepe: info@rea.go.tz