Kwa Ushirikiano na Benki ya Dunia Kupitia International Finance Corporation (IFC)
Serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania imezindua tovuti inayotoa taarifa za fursa na taratibu za uwekezaji kwenye miradi midogo ya umeme nje ya gridi ya Taifa.
Uzinduzi wa tovuti hiyo ulifanyika tarehe 11 Agosti, 2016 katika Ofisi za Benki ya Dunia Tanzania. Lengo la tovuti hiyo ni kutoa taarifa ambazo zitawawezesha waendelezaji wa miradi ya nishati bora vijijini, wawekezaji mbalimbali pamoja na wadau wengine kupata taarifa sahihi ambazo zitachangia katika kuongeza wigo wa usambazaji na upatikanaji wa nishati bora vijijini.
Tovuti hiyo inatoa taarifa za kina kwa waendelezaji na wawekezaji kwenye miradi midogo ya nishati jadidifu nchini Tanzania.
Uanzishwaji wa tovuti hii umefanyika chini ya mradi wa SREP (Scaling-Up Renewable Energy Program) ambao unachochea uwekezaji kwenye nishati jadidifu ikijumuisha miradi midogo ya umeme (minigrids).
Tovuti hiyo, www.minigrids.go.tz inasimamiwa na kuhifadhiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na taarifa zake zinaratibiwa kwa ushirikiano wa uwakilishi wa wadau wengine ambao ni Wizara ya Nishati na Madini (MEM), EWURA, NEMC, TAREA, TBS pamoja na TANESCO.
Imeandaliwa na:
Jaina D. Msuya
Afisa Habari na Elimu kwa Umma
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mawasiliano Towers, Ghorofa ya 2
Barabara ya Sam Nujoma
S. L. P 7990
Dar es Salaam, Tanzania
Barua Pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 22 2412001, +255 22 2412002, +255 22 2412003
Nukushi: +255 22 2412007