Waziri wa Nishati Aweka Ukomo wa Kuagiza Vifaa Vya Ujenzi wa Miradi ya Nishati
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Merdad Kalemani ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme (TANESCO) kuweka mpango ambao utawezesha vifaa vyote vinavyotumika katika ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme vinatengenezwa hapa nchini.
Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo katika Mkutano wake uliojumuisha viongozi wa Wizara, Bodi ya Nishati Vijijini (REB) pamoja na Menejimenti ya REA uliofanyika tarehe 21 Oktoba 2019 katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo katika Mji wa Serikali wa Mtumba Jijini Dodoma. “Accessories kutoka nje ya nchi ni changamoto na zina mlolongo mrefu kutoka kuagizwa mpaka kufika nchini hivyo REA na TANESCO mjipange, kufikia tarehe 31 Desemba 2019 itakuwa mwisho wa kuagiza vifaa hivyo kutoka nje ya nchi” alisisitiza.
Waziri aliwaagiza REA na TANESCO kuyashawishi makampuni yanayozalisha vifaa yaliyopo nje ya nchi kufungua viwanda hivyo hapa nchini na kwamba tayari kuna kampuni zimeonesha nia ya kuanzisha viwanda hivyo nchini Tanzania. Aidha, Mh. Waziri aliitaka REB na Menejimenti ya REA kukutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuweka mkakati wa pamoja ambao utasaidia kutolewa kwa wakati bandarini vifaa ambavyo vimeagizwa kutoka nje ya nchi ili kuweza kukamilisha miradi ya kusambaza umeme kwa wakati. “Wekeni mkakati wa pamoja na TRA kwa vifaa vyote vya miradi ya REA ambavyo vinaagizwa kutoka nje ya nchi visichelewe kutolewa bandarini”, alisisitiza.
Katika Mkutano huo, Mhe. Dkt. Merdad Kalemani amekubaliana na Bodi ya Nishati Vijijini kuwaweka katika uangalizi maalum wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza ambao utekelezaji wao umekuwa ukisuasua.
Dkt. Kalemani aliagiza ufanyike uchambuzi wa kina wa utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya III Mzunguko wa I ili kuwatambua wakandarasi wanaofanya vizuri na wale ambao utekelezaji wao umekuwa ni wa kusuasua ili waweze kusimamiwa kwa karibu kwa kuwekwa katika uangalizi maalum hatimaye waweze kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme kwa muda unaotakiwa.
Mh. Waziri alisisitiza kuongeza usimamizi kwa wakandarasi ili kila mkandarasi aweze kuwasha umeme katika vijiji vitatu kila wiki na kuwa hilo litafanikiwa endapo wakandarasi wataongeza idadi ya wafanyakazi katika maeneo ya mradi. Aidha, aliagiza kuwa ikifika Desemba tarehe 31 Desemba 2019 kazi zote za marekebisho ya Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya II ambao ulikamilika Mwaka 2016 ziwe zimekamilika na makabidhiano yawe yamefanyika.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri aliagiza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya III Mzunguko wa II uanze Mwezi Januari Mwaka 2020 na kuharakisha maandalizi ya miradi ya ujazilizi katika vijiji ambavyo vimefikiwa na miundombinu ya umeme. Hata hivyo, alionya kuwa ufanyike uhakiki wa kina wa vijiji ambavyo vitapelekewa miradi ya umeme ili kujua mahitaji halisi.
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Leonard Masanja alisema kuwa changamoto kubwa ya utekelezaji wa mradi unaoendelea hivi sasa inatokana na baadhi ya wakandarasi kuwa nyuma ya utekelezaji hivyo kusababisha vijiji vingi kutopelekewa umeme. “Tunaandaa Mzunguko wa II wa mradi tukiwa na madeni na muda uliobaki ni vigumu kwa wakandarasi kukamilisha kazi” alisisitiza.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la LAPF, Ghorofa ya 7
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507