Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Mhe. Shaib Kaduara ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuendelea kuhakikisha huduma za Nishati zinafika katika maeneo yote ya Vijiji Tanzania Bara.
Ametoa pongezi hizo Jijini Dar es Salaam Oktoba 25, 2024 alipotembelea Banda la Wakala kabla ya kufunga Kongamano la 10 la Jotoardhi (ARGeo-C10).
Mhe. Kaduara aliisisitiza REA kuhakikisha inaongeza nguvu katika suala la uhamasishaji ili kuwezesha wananchi umuhimu wa kubadilika na kuachana na matumizi ya nishati ambazo sio safi na salama kwa afya zao na kwa mazingira.
"Hongereni mnafanya kazi nzuri, muhimu ni kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi waelewe umuhimu wa kubadilika na kuachana na matumizi ya Nishati chafu," alielekeza.
Awali akitoa maelezo ya majukumu ya REA, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage alisema Wakala unatekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) ambao ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Mwijage amesema REA inatekeleza program mbalimbali ili kuhakikisha wananchi hususan wa maeneo ya vijijini wanapunguza na baadae kuachana kabisa na matumizi ya nishati chafu za kupikia ikiwemo kuni na mkaa.
"Tumeingia makubaliano na wasambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia ambapo kwa mwaka huu 2024/2025 tunatoa mitungi zaidi ya laki nne kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50," amesema.
Ameongeza kuwa majadiliano yanaendelea na watengenezaji wa majiko banifu ambapo kwa awamu ya kwanza majiko yapatayo 200,000 yatatolewa kwa bei ya ruzuku ya hadi asilimia 75.
Aidha alizungumzia suala la usambazaji wa umeme maeneo ya vijijini ambapo alisema hadi kufikia Desemba mwaka huu vijiji vyote Tanzania Bara vitakuwa vimeunganishwa na umeme.
"Kwa sasa zaidi ya asilimia 98 ya vijiji vyote Tanzania Bara vimeunganishwa na umeme na sasa tumeanza kusambaza umeme vitongojini," amesema Mhandisi Mwijage.
Mhandisi Mwijage amesema Wakala unashiriki Kongamano la 10 la Jotoardhi kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya Nishati Jadidifu hasa ikizingatiwa kuwa Jotoardhi ni aina moja ya nishati jadidifu.
Amesema REA inafadhili miradi mbalimbali ya Nishati Jadidifu na kwamba kwa miradi ya upepo, jua na maporomoko ya maji Watanzania wengi wamejitokeza kushirikiana na Serikali kuitekeleza.
Hata hivyo amesema kwa Nishati ya Jotoardhi bado wananchi hawajawa na mwamko wa kutosha na kwamba kupitia kongamano na uhamasishaji unaofanywa na Serikali wanananchi watahamasika.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma