Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi wa umma.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy ameelekeza hayo Novemba 26, 2024 wakati wa mkutano na watumishi wote wa wakala.
"Majukumu yetu ya msingi ni kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Nishati Vijijini na Kuwezesha miradi ya Nishati Vijijini na majukumu haya tutayafanya kwa ufanisi endapo tutaendelea kuzingatia miongozo iliyopo," amesisitiza Mha. Saidy.
Amesema wakala unaendelea kufanya vizuri katika majukumu iliyokasimiwa na Serikali na ametoa wito kwa watumishi wote kuendelea kushirikiana kuhakikisha majukumu hayo yanatekelezwa kwa ufanisi na tija inapatikana.
Amepongeza watumishi kwa kuendelea kujituma na amesisitiza waendelee na moyo huo ili kutimiza dhamira ya Serikali.
"Serikali yetu inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetuamini katika kuwafikishia wananchi wake Nishati tusikubali kukwama kwa namna yoyote," ameelekeza.
Katika kikao hicho, watumishi walipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya utekelezaji wa majuku yao sambamba na namna bora ya kuendelea kuboresha maeneo yao ya kazi.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma