Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Viongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Watumishi wameshiriki Bonanza la Nishati lililoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko lililofanyika leo Julai 27 Jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya bonanza hilo, Dkt. Biteko amewakumbusha Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuiishi Kauli Mbiu ya Sekta ya Nishati ambayo ni Maneno Kidogo Vitendo zaidi ili kuweza kutoa huduma iliyobora kwa wananchi.
“Sekta ya Nishati ni muhimu kwenye ujenzi wa uchumi wa nchi yetu na tufahamu kwamba Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatutegemea sisi ili kuweza kutoa huduma hii muhimu kwa wananchi, hivyo watumishi tupendane, tushirikiane na kufanya kazi kwa bidi zaidi ili kusukuma mbele gurudumu la Nishati.” Amesema Dkt.Biteko
Kuhusu Bonanza hilo la Nishati, Dkt. Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na morali waliyokuwa nayo Watumishi ambao walishiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali na kuahidi kuwa huo utakuwa ni utaratibu wa kila mwaka mara baada ya kufanyika kwa Bunge la Bajeti.
Aidha, amewapongeza Watumishi walioshinda michezo mbalimbali katika Bonanza hilo pamoja Viongozi wa Wizara ya Nishati walioratibu Bonanza husika kwa mafanikio.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu , Mhe. Jenista Mhagama ameeleza kufurahishwa na jinsi Bonanza la Nishati lilivyofanikiwa na kusema kuwa huo ni muitikio wa nia ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya njema na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo dawa yake kubwa ni mazoezi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuanzisha Bonanza hilo ambalo amesema linadumisha upendo miongoni mwa Watumishi, umoja, kuwawezesha wafanyakazi kufahamiana zaidi na kuwaimarisha Watumishi.
Amesema kuwa, anaamini Watumishi wamepata motisha ya kazi kupitia bonanza hilo pamoja na hamasa ya kujipanga na kujiimarisha kwa ajili ya michezo inayofuata.
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amemshukuru Dkt. Biteko kwa wazo lake la Bonanza ambalo limeleta hamasa kubwa kwa watumishi na kuahidi kwamba Bonanza hilo sasa litafanyika kila mwaka.
Amesema Taasisi zote chini ya Wizara Nishati zimeshirki bonanza hilo ikiwemo Kampuni Tanzu za Taasisi hizo.
Imetolewa na:
Iddy M. Mwema
imwema@rea.go.tz
Afisa Habari
REA