Social Links Search User Login Menu
Tools
Close
Close
Dkt. Biteko Aimwagia Sifa REA, Ataka Taasisi Zingine Ziige
Frank A. Mugogo 900

Dkt. Biteko Aimwagia Sifa REA, Ataka Taasisi Zingine Ziige

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kukamilisha lengo la usambazaji Umeme katika Vijiji 12,318 Nchini na kwa umahiri wake katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Ametoa pongezi hizo Agosti 22, 2025 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi majiko yanayotumia Nishati Safi kwa Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

"REA mmefanya kazi kubwa, tunawapongeza kwa kuibeba vyema ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Nishati Safi ya Kupikia sambamba na kukamilisha kwa wakati lengo la kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 na sasa mnasambaza umeme vitongojini," alipongeza Mhe. Dkt.Biteko.

Aliipongeza Bodi ya Nishati Vijijini (REB) chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu kwa umahiri wake katika katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kasi na viwango sambamba na kumpongeza Mtendaji Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy kwa kusimamia vyema watendaji walio chini yake.

Alibainisha kuwa Wizara ya Nishati inao utaratibu wa kupima utendaji wa kila taasisi inayoisimamia na kwamba REA ni taasisi ambayo imefanya vizuri mara tatu mfululizo kuatika tathmini hiyo ya utendaji wa taasisi ambayo hufanyika kila baada ya miezi mitatu.

"Katika robo ya kwanza ya upimaji wa utendaji REA ilishinda nafasi ya kwanza, robo iliyofuatia REA ilichukua nafasi ya pili na robo hii iliyomalizika hivi karibuni REA imeshika nafasi ya kwanza kwa taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati, kazi mnayofanya imewezekana kwasababu ya utulivu wa taasisi, mnayo Bodi nzuri na uongozi mzuri," alibainisha Mhe. Dkt. Biteko.

Aliongeza kuwa miradi yote inayosimamiwa na REA inakamilika kwa wakati na kwa ubora mzuri na kwamba hajawahi kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa wafadhili wa miradi na mara zote wamekuwa wakimpatia sifa njema za utendaji wa Wakala.

"Nampongeza Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy kwa uongozi wake amewafanya watumishi wa REA wajione wa daraja la juu, hajawagawa kwa makundi hana wapambe ndio maana huwezi kusikia kelele, tuendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vyema miradi tuliyokabidhiwa," alisema Mhe.Dkt. Biteko.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu alisema Wakala unaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo. 

"Ombi langu zoezi hili itapendeza na kuleta matokeo chanya endapo taasisi zote zitatoa majiko haya kwa watumishi; hii italeta chachu kwa Wizara zingine na taasisi mbalimbali kufanya vivyo hivyo na itaongeza kasi ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais ya kuhakikisha 80% ya Watanzania wanahamia kutumia Nishati Safi ifikapo mwaka 2034 na hili linawezekana," alisema Balozi Kingu.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Nishati Safi ya Kupikia, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alimshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Mashaka Biteko kwa miongozo yake ya namna bora ya kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kufikia lengo la 80% ifikapo mwaka 2034.

Mhandisi Saidy aliainisha mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa kupitia REA na alitaja baadhi ya miradi ikiwemo kujenga mifumo ya gesi asilia Lindi na Pwani na kwamba hadi sasa wananchi 460 wamefikiwa kati ya 980 waliolengwa, kufunga mifumo katika Jeshi la Magereza ambapo magereza yote 129 yamefikiwa sambamba na kufunga mifumo katika kambi 22 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Mbali na miradi hiyo, Mhandisi Saidy alisema REA imeliwezesha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kiasi cha shilingi bilioni 3 kujenga mtambo wa kuzalisha mkaa mbadala maarufu kama 'rafiki briquettes', majiko banifu 200,000 vijijini kusaidia wananchi ambao ni ngumu kufikiwa na nishati safi zingine.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma

Share

Print
«September 2026»
MonTueWedThuFriSatSun
31123456
789
Rea Yawajengea Uwezo Waendelezaji wa Miradi Midogo ya Umeme Unaozalishwa na Maporomoko ya Maji

Rea Yawajengea Uwezo Waendelezaji wa Miradi Midogo ya Umeme Unaozalishwa na Maporomoko ya Maji

IRINGA, Nyanda za Juu Kusini

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini kwa kuendesha mafunzo maalum ya wiki moja yaliyolenga kujenga uwezo wa waendelezaji wa miradi midogo ya uzalishaji wa umeme unaotokana na maporomoko ya maji (Small Hydropower).

Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 7 Septemba, 2026 katika Hoteli ya Sunset mkoani Iringa, yamewakutanisha waendelezaji wa miradi (Developers) zaidi ya 15, hususan kutoka maeneo ya Nyanda za Juu Kusini. Lengo kuu ni kuwajengea uwezo wa kiufundi ili kuongeza ubora wa miradi yao ili iweze kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, tarehe 9 Septemba, 2026, Kaimu Meneja wa Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya, alisema kuwa REA haishii tu kutoa msaada wa upatikanaji wa nishati vijijini, bali inajikita pia katika kuongeza ujuzi wa wataalamu wa ndani.

"Kuongeza ujuzi kwa waendelezaji hawa kutasaidia kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na ubora unaohitajika. Hatua hii itaongeza idadi ya miradi inayofikia vigezo vya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, kuongeza uzalishaji wa umeme, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini," alisema Mhandisi Yesaya.

Mafunzo hayo yameendeshwa kwa ushirikiano kati ya REA na Wataalamu kutoka Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Maeneo yaliyofundishwa ni pamoja na usanifu wa miradi, upembuzi yakinifu, sayansi ya maji (hydrology), uhandisi wa umeme na elektroniki, pamoja na uendeshaji na matengenezo ya mitambo.

Mbali na mafunzo, REA imebainisha kuwa imekuwa ikisaidia waendelezaji hao kupitia ruzuku za ujenzi, maandalizi ya maandiko ya miradi na usanifu.

Aidha, Wakala huo upo katika mchakato wa kuandaa mfumo wa mikataba ya muda mrefu (Framework Contract) na taasisi za elimu ili kutoa mafunzo endelevu kwenye nishati jadidifu ikiwemo nishati ya jua na mifumo ya gesi vunde.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wamepongeza mafunzo hayo; akizungumza na Wanahabari, Mhandisi Denis Makoyi kutoka kampuni ya Africa Power Investment, alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa mkubwa wa kiufundi katika hatua za utekelezaji wa miradi. Naye Lutengano Kigola kutoka mradi wa Nyalawa Hydropower, aliongeza kuwa mafunzo hayo yanathibitisha kuwa Tanzania ina wataalamu wa ndani wenye uwezo mkubwa wa kuendeleza miradi ya umeme wa maji.

  • MWISHO –

 

Read more
10111213
14
REA Yaendelea Kuwezesha Miradi ya Umeme wa Maji Nyanda za Juu Kusini

REA Yaendelea Kuwezesha Miradi ya Umeme wa Maji Nyanda za Juu Kusini

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuwezesha waendelezaji wadogo wa miradi ya uzalishaji wa umeme unaotokana na maporomoko ya maji (Small Hydropower) katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kutoa fedha, msaada wa kitaalamu na mafunzo, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa nishati nchini.

Read more
151617181920
21222324252627
2829301234
567891011

Archive

Contact Us

E-Mail
General Information:  info@rea.go.tz
Director General:  dg@rea.go.tz
Procurement (PMU):  pmu@rea.go.tz
Webmaster:  webmaster@rea.go.tz

Mailing Address

Director General
Rural Energy Agency - REA
REA Building
28 Medeli Street
P. O. Box 2153
Dodoma, Tanzania

Phone & Fax

Tel: +255 26 2323504, +255 26 2323506
+255 26 2323507
Fax: +255 26 2323507

Time Zone

Please note that we are based in Tanzania, Time zone (GMT+03:00). Although we may not be in office at times convenient for all international enquiries, we do monitor our e-mail outside normal office hours.

Back To Top