Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza rasmi safari ya kupeleka umeme katika visiwa vyote Tanzania Bara huku ikiwahakikishia wananchi hao kuwa wote watafikiwa.
Akizungumza wakati wa ziara ya Wabia wa Maendeleo walipotembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi, Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amesema kuwa mradi huo ni dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata nishati ya umeme kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Ziara hiyo ambayo imefanyika katika kisiwa cha Musira kilichopo Wilaya ya Bukoba Mjini, mkoani Kagera, viongozi mbalimbali wa Serikali waliambatana na Wabia hao wa Maendeleo ambao Serikali imekuwa ikishirikiana na kuwezesha upatikanaji wa nishati bora vijijini. Wabia hao ni Benki ya Dunia, Serikali ya Norway, Serikali ya Sweden, Umoja wa Ulaya, AFD na ADB.
“Tumekuja kwa ajili ya kufanya vikao vya tathmini ya miradi inayotekelezwa lakini pia hatutafanya vikao tuu, pia tunatembelea miradi inayotekelezwa pamoja na Wabia wa Maendeleo na hapa Musira tumekuja kuona utekelezaji wa mradi wa mifumo ya umeme jua inayofungwa kwa wananchi.
Huku kuna wateja 191 na wateja 56 tayari wameshapata umeme. Mimi kama Mwenyekiti wa Bodi najivunia utekelezwaji wa miradi inayotekelezwa na REA. Hii yote ni dhamira ya Serikali kuhakikisha hakuna mwananchi popote alipo anabaki kwenye giza,” amesema Mhe. Balozi Kingu.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila amesema kuwa serikali imekuwa ikitumia masuluhisho mbalimbali kufikisha umeme kwa wananchi ikiwa ni kwa njia ya kusambaza umeme kawaida au kwa kutoa ruzuku kwenye mifumo ya umeme jua kwa wananchi wanaoishi visiwani ili kuweza kubadilisha maisha yao.
Awali akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa mradi huo wenye zaidi ya gharama ya shilingi Bilioni 8 unatarajiwa kunufaisha wananchi wote waishio katika visiwa kwa kupatiwa mifumo ya umeme jua kwa bei ya ruzuku.
Amesema kuwa zaidi ya mikoa 7 inatarajiwa kunufaika na mradi huo ambapo mifumo zaidi ya 20,000 inatarajiwa kufungwa katika visiwa 118 ambavyo vitapatiwa mifumo hiyo.
“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na maziwa na bahari na ndani ya maeneo hayo kuna visiwa ambapo kuna wananchi wanaishi na siyo rahisi kupeleka umeme wa kawaida kwenye kila kisiwa kutokana na gharama kuwa kubwa na serikali kupitia na REA imekuja na mpango maalum wa kufunga mifumo ya umeme jua visiwani. Mradi huu utaenda kuhakikisha visiwa vyote vinapata umeme,” amefafanua Mhandisi Saidy.
Amewahamasisha wananchi kutunza miundombinu hiyo na kuchangamkia fursa za uwepo wa mradi huo ambapo serikali imetoa ruzuku ya hadi asilimia 75 ya kufungiwa mifumo hiyo ya umeme jua.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema kuwa kwa Mkoa wa Kagera jumla ya shilingi Bilioni 2.1 zinatarajiwa kutumika kupeleka mifumo ya umeme jua katika visiwa vilivyopo katika Mkoa huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Rafiki Energy, Eliud Mjuni ambayo inayotekeleza mradi wa kufunga mifumo ya umeme jua katika kisiwa hicho amesema kuwa tayari wamefanikiwa kufunga mifumo ya umeme jua zaidi ya 20 huku wakiwafikia wateja zaidi ya 56.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma