UZINDUZI WA MRADI WA UMEME VIJIJINI AWAMU YA TATU MKOA WA SIMIYU
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umezindua utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Simiyu. Mgeni rasmi Katika uzinduzi huo uliofanyika tarehe 14/07/2017 katika kijiji cha Nangale, Kata ya Ndolelezi, Wilaya ya Itilima alikuwa ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani.
Mradi huu unajumuisha vipengele-mradi vitatu vya Grid Extension, Densification ambayo inalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vijiji ambavyo vimefikiwa na miundombinu ya umeme lakini baadhi ya vijiji na vitongoji havikuunganishiwa umeme. Kipengele-mradi cha tatu kinahusisha usambazaji wa nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi.
Utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Simiyu utahusisha vipengele vyote vitatu. Mradi huu utatekelezwa kwa vipindi viwili tofauti. Sehemu ya awali itahusisha upelekaji umeme katika vijiji 152 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 33.47. Utekelezaji wa sehemu hii ya kwanza umeanza Mwezi Februari 2017 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 2019. M/s White City Contractors Limited na Guangdong Limited ni wakandarasi watakaotekeleza Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Mkoa Simiyu.
Aidha, sehemu ya pili ya mradi huu wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu itaanza kutekelezwa baada ya sehemu ya kwanza kukamilika Mwaka 2019 ambapo vijiji 195 vitapatiwa umeme na hivyo kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Simiyu ifikapo Mwaka 2021.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mawasiliano Towers, Ghorofa ya 2
Barabara ya Sam Nujoma
S. L. P 7990
Dar es Salaam, Tanzania
Barua Pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 22 2412001, +255 22 2412002, +255 22 2412003
Nukushi: +255 22 2412007