Wakandarasi wa REA Wahimizwa Kuunganishia Wateja Umeme kwa Kutumia UMETA
Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya III Mzunguko wa I wameagizwa kuwaunganisha wananchi walio katika eneo la mradi kwa kutumia kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho ni mbadala wa kufunga mfumo wa nyaya katika nyumba (wiring) ili kuepuka kuruka nyumba zilizofikiwa na miundombinu ya umeme.
Agizo hilo lilitolewa tarehe 23 Oktoba 2019 na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Styden Rwebangira katika kikao cha majumuisho ambacho kilihudhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini, Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini, Wakandarasi na Mameneja wa TANESCO wa wilaya zote za Mkoa wa Tanga baada ya ukaguzi wa utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Tanga ambapo aliwataka wakandarasi wahakikishe wanagawa UMETA 250 za bure ambazo zimetolewa na Serikali kwa wananchi wote ambao hawajafunga mfumo wa nyaya katika nyumba zao.
Mhandisi Rwebangira alisema kwa ujumla wameridhishwa na kazi ya utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Tanga. “Tunaridhishwa na utendaji wa wakandarasi, changamoto ni kwamba vifaa vya UMETA havifungwi kwenye nyumba za wananchi” aliongeza.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine ambayo wameibaini ni uhaba wa nyaya zinazotumika katika ujenzi wa miundombinu ya kusambazia umeme na kuwa suala hilo linafuatiliwa na Bodi ya NIshati Vijijini pamoja na Waziri wa Nishati ambapo kutakuwa na kikao cha watengenezaji wa nyaya tarehe 29 oktoba 2019 ili kuweka mkakati wa upatikanaji wa nyaya na kuwawezesha wakandarasi kukamilisha mradi kwa wakati.
Mhandisi Rwebangira aliwahimiza wakandarasi wote wanaotekeleza mradi huo nchini kukamilisha kazi ifikapo tarehe 31 Desemba 2019 ili kutoa nafasi kwa mzunguko wa pili wa mradi huo kuanza Mwezi Januari 2020 bila ya viporo vya kazi za mzunguko wa kwanza. Aliwatahadharisha wakandarasi ambao hawatakamilisha kazi wanaweza wakakosa fursa ya kuomba tena kazi za kusambaza umeme katika mzunguko wa pili zitakapotangazwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu aliwahimiza wakandarasi kuhakikisha kuwa wamepeleka vifaa vyote katika maeneo ya mradi kabla msimu wa mvua haujaanza ili kuepuka usumbufu wa kusafirisha vifaa hivyo kipindi cha mvua.
Wakandarasi walisema wamepokea agizo la kukamilisha mradi ifikapo 31 Desemba 2019 na kuiomba REB ihakikishe kuwa nyaya zinazotumika katika ujenzi wa miundombinu ya kusambazia umeme zinapatikana kutoka kwa wazalishaji wa ndani kwa wakati. Msimamizi wa Mradi wa Kampuni ya Derm Electric, Mhandisi Aziz Msuya alisema kuwa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 83.5 na kuwa nguzo zimesimikwa katika vijiji 24 na kimebaki kijiji kimoja tu kusimikwa nguzo hadi kufikia tarehe hiyo. Alisema changamoto ni jiografia ambayo inasumbua kusafirisha nguzo katika maeneo ya milimani.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Njarita, Michael Njarita alisema kuwa wamefikia asilimia 67.8 ya utekelezaji wa mradi na kuwa changamoto kubwa ni upatikanaji wa nyaya na mabadiliko ya hali ya hewa. “Lengo la kumaliza mradi ifikapo tarehe 31 Desemba 2019 lipo palepale, tutajitahidi kumaliza kwa wakati” alisema.
Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tanga, Bw. Sebastian Masanja alisema upatikanaji wa huduma ya umeme vijijini unachochea ukuaji wa uchumi kwa kuongeza ajira katika sekta isiyo rasmi na kutoa fursa kwa vijana wengi kujiari kwa kuanzisha biashara za kuchomelea vyuma, gereji, maduka, salon za kunyolea nywele na mabanda ya kuonesha mipira.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la LAPF, Ghorofa ya 7
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507