Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa shilingi bilioni 25.8 wa kusambaza umeme katika vitongoji 159 utakaonufaisha kaya 5,116 mkoani Lindi.
Meneja Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme wa REA, Mhandisi Deogratius Nagu amebainisha hayo Januari 27, 2026 mkoani Lindi wakati wa kumtambulisha Mkandarasi Mzawa aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo, Kampuni ya Jaitech Co Ltd kwa ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
“Tunamshukuru Rais Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha shilingi 25,826,594,700.00 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 159 mkoani hapa na leo hii tumefika hapa kumtambulisha Mkandarasi na maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza,” amesema Mhandisi Nagu.
Akizungumzia hali ya usambazaji umeme mkoani humo, Mhandisi Nagu amesema kuwa,vijiji vyote 523 vimefikishiwa umeme na kwamba hadi sasa vitongoji 1,831 vimefikishiwa umeme kati ya vitongoji 2,402.
“REA inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vilivyobaki, hivi tunavyozungumza Wakandarasi wanaendelea na kazi na hadi sasa katika vitongoji hivyo vilivyobaki vitongoji 378 vipo kwenye mpango wa kufikishiwa umeme,” amebainisha.
Amesema, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini viwe vimefikishiwa nishati ya umeme na kwamba REA ikiwa na dhamana hiyo imejipanga kikamilifu kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati kufikia dhamira hiyo.
Aidha,Mhandisi Nagu ametoa wito kwa wananchi watakaopitiwa na mradi kuhakikisha wanatoa ushirikiano ili kumuwezesha Mkandarasi kutekeleza kazi ndani ya muda na kwa ubora unaopaswa na kwamba mradi huo unazo faida lukuki kuanzia hatua za awali za utekelezaji hadi hapo utakapokamilika.
Pia, Mhandisi Nagu ameiomba Ofisi ya Mkoa kushirikiana na REA kufikisha elimu na taarifa sahihi kwa wananchi kuwa hakutokuwa na fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yatapitiwa na mradi hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni fursa ya kiuchumi na kijamii.
“Tunaomba ushirikiano kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kurahisisha utekelezaji wa mradi ikiwemo kuruhusu mradi kukatiza katika baadhi ya maeneo ya misitu sambamba na kuwa na miundombinu wezeshi kuruhusu kusafirisha vifaa vya mradi maeneo mbalimbali atakapokuwa mkandarasi,” amesema Mha. Nagu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Katibu Tawala wa mkoa huo, Zuwena Omari ameipongeza REA kwa kuendelea kuenzi kwa vitendo dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufikisha maendeleo kwa wananchi.
Amesema, Ofisi ya Mkoa wa Lindi itatoa ushirikiano kwa Mkandarasi muda wote wa utekelezaji wa mradi na alimtaka Mkandarasi kuhakikisha anatoa taarifa endapo atakutana na changamoto yoyote.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Jaitech Co Ltd, Isihaka Kibode ameishukuru Serikali kwa kupata kazi na ameahidi kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwamba atashirikiana karibu na viongozi na wananchi wa maeneo ya mradi.