Social Links Search User Login Menu
Tools
Close
Close
Rais Samia Awafuta Machozi ya Kuni Akina Mama Nchini
Frank A. Mugogo 944

Rais Samia Awafuta Machozi ya Kuni Akina Mama Nchini

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza mradi wa shilingi 9,400,799,626.7 wa kusambaza majiko yaliyoboreshwa maarufu kama majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 80 hadi 85 kote nchini.

Hayo yamesemwa Agosti 4, 2025 na mwakilishi wa REA Mkoani Morogoro, Mhandisi Cecilia Msangi wakati akimtambulisha Mtoa huduma aliyeshinda zabuni ya kusambaza majiko hayo Mkoani humo, kampuni ya Burn Manufacturing Tanzania Ltd katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

"Wakala unatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia miradi mbalimbali ikiwemo huu wa kusambaza majiko banifu ambao rasmi leo hii tupo hapa kuutambulisha kwa wananchi wa Morogoro," alisema Mha. Msangi.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kampeni hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo alisema kwa jitihada zake binafsi hatua mbalimbali zimechukuliwa hususan za kuwanusuru akina mama kutokana na madhara ya moshi wa kuni sambamba na uhifadhi wa mazingira.

Alisema Rais Samia alitoa maelekezo mahususi ya kuhakikisha wananchi wanawezeshwa ili kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kupikia ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umeelekeza ifikapo Mwaka 2034; 80% ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumza juu ya utekelezaji wa mradi kwa Mkoa wa Morogoro, Mha. Msangi alisema jumla ya majiko banifu 8,366 yatatolewa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 14,694 kwa kila jiko.

"Kwa bei ya kawaida kabla ruzuku jiko hilo lilikuwa likiuzwa shilingi 73,468.36 na sasa baada ya kupokea kwa ruzuku ya 80% jiko hilo litauzwa kwa shilingi 14,694 tu," alibainisha Mhandisi Msangi.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mussa Mussa alipongeza jitihada za REA na alisema kuwa manufaa yatakayopatikana kutokana na mradi huo ni makubwa kuliko hata inavyotarajiwa.

"Haya majiko namna yalivyosanifiwa yanatumia mkaa kidogo na pia yanatunza joto kwa muda mrefu, hivyo inakwenda kumpunguzia mwananchi gharama za mkaa na kumuokolea muda," alisisitiza Katibu Tawala, Musa.

Aidha, Meneja wa Kampuni ya Burn Manufacturing Tanzania Ltd, John Mtui alisema kampuni yao imeshinda zabuni ya kusambaza majiko banifu 39,286 katika Mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Kagera na Tabora ambayo ni sawa na shilingi 2,309,022,392.77.
"Hapa Morogoro tutasambaza jumla ya majiko 8,366 katika Wilaya za Gairo, Kilombero, Kilosa, Malinyi, Morogoro Vijijini, Ulanga na Mvomero ambapo kila wilaya itapata majiko 1,196," alisema Mtui.

REA inatekeleza miradi mbalimbali nchini kwa kuwezesha na kuelimisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama kwa afya zao na mazingira kwa ujumla.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma

Share

Print
«September 2026»
MonTueWedThuFriSatSun
31123456
789
Rea Yawajengea Uwezo Waendelezaji wa Miradi Midogo ya Umeme Unaozalishwa na Maporomoko ya Maji

Rea Yawajengea Uwezo Waendelezaji wa Miradi Midogo ya Umeme Unaozalishwa na Maporomoko ya Maji

IRINGA, Nyanda za Juu Kusini

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini kwa kuendesha mafunzo maalum ya wiki moja yaliyolenga kujenga uwezo wa waendelezaji wa miradi midogo ya uzalishaji wa umeme unaotokana na maporomoko ya maji (Small Hydropower).

Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 7 Septemba, 2026 katika Hoteli ya Sunset mkoani Iringa, yamewakutanisha waendelezaji wa miradi (Developers) zaidi ya 15, hususan kutoka maeneo ya Nyanda za Juu Kusini. Lengo kuu ni kuwajengea uwezo wa kiufundi ili kuongeza ubora wa miradi yao ili iweze kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, tarehe 9 Septemba, 2026, Kaimu Meneja wa Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya, alisema kuwa REA haishii tu kutoa msaada wa upatikanaji wa nishati vijijini, bali inajikita pia katika kuongeza ujuzi wa wataalamu wa ndani.

"Kuongeza ujuzi kwa waendelezaji hawa kutasaidia kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na ubora unaohitajika. Hatua hii itaongeza idadi ya miradi inayofikia vigezo vya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, kuongeza uzalishaji wa umeme, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini," alisema Mhandisi Yesaya.

Mafunzo hayo yameendeshwa kwa ushirikiano kati ya REA na Wataalamu kutoka Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Maeneo yaliyofundishwa ni pamoja na usanifu wa miradi, upembuzi yakinifu, sayansi ya maji (hydrology), uhandisi wa umeme na elektroniki, pamoja na uendeshaji na matengenezo ya mitambo.

Mbali na mafunzo, REA imebainisha kuwa imekuwa ikisaidia waendelezaji hao kupitia ruzuku za ujenzi, maandalizi ya maandiko ya miradi na usanifu.

Aidha, Wakala huo upo katika mchakato wa kuandaa mfumo wa mikataba ya muda mrefu (Framework Contract) na taasisi za elimu ili kutoa mafunzo endelevu kwenye nishati jadidifu ikiwemo nishati ya jua na mifumo ya gesi vunde.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wamepongeza mafunzo hayo; akizungumza na Wanahabari, Mhandisi Denis Makoyi kutoka kampuni ya Africa Power Investment, alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa mkubwa wa kiufundi katika hatua za utekelezaji wa miradi. Naye Lutengano Kigola kutoka mradi wa Nyalawa Hydropower, aliongeza kuwa mafunzo hayo yanathibitisha kuwa Tanzania ina wataalamu wa ndani wenye uwezo mkubwa wa kuendeleza miradi ya umeme wa maji.

  • MWISHO –

 

Read more
10111213
14
REA Yaendelea Kuwezesha Miradi ya Umeme wa Maji Nyanda za Juu Kusini

REA Yaendelea Kuwezesha Miradi ya Umeme wa Maji Nyanda za Juu Kusini

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuwezesha waendelezaji wadogo wa miradi ya uzalishaji wa umeme unaotokana na maporomoko ya maji (Small Hydropower) katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kutoa fedha, msaada wa kitaalamu na mafunzo, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa nishati nchini.

Read more
151617181920
21222324252627
2829301234
567891011

Archive

Contact Us

E-Mail
General Information:  info@rea.go.tz
Director General:  dg@rea.go.tz
Procurement (PMU):  pmu@rea.go.tz
Webmaster:  webmaster@rea.go.tz

Mailing Address

Director General
Rural Energy Agency - REA
REA Building
28 Medeli Street
P. O. Box 2153
Dodoma, Tanzania

Phone & Fax

Tel: +255 26 2323504, +255 26 2323506
+255 26 2323507
Fax: +255 26 2323507

Time Zone

Please note that we are based in Tanzania, Time zone (GMT+03:00). Although we may not be in office at times convenient for all international enquiries, we do monitor our e-mail outside normal office hours.

Back To Top