Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) yalifanyika Mkoani Lindi katika Viwanja vya Ngongo kuanzia tarehe 01/08/2016 hadi 08/08/2016. Ujumbe wa maonesho hayo ulikuwa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Nguzo ya Maendeleo, Kijana Shiriki Kikamilifu “Hapa Kazi tu”.
Katika maonesho hayo Wakala ulishiriki pamoja na wadau ambao ni:
- EFFORT - Walioonesha teknolojia ya kutengeneza mkaa mbadala;
- Moody Solar - Walioonesha teknolojia ya Umeme Jua;
- Davis & Shertilif - Walioonesha teknolojia za Vifaa vya umeme jua (zikilenga pampu ya kumwagilia maji);
- Oryx Gas Ltd - Walioonesha teknolojia ya Gesi ya kupikia majumbani; na
- Ok Electrical and Electronics Services LTD - Walioonesha teknolojia ya vifaa vya usambazaji wa umeme vijijini.
Katika maonesho hayo, Wakala ulipata fursa ya kuelezea mpango wake wa kusambaza umeme vijijini na kuonesha picha za wanufaika wa miradi ya REA katika mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na mikoa mingine (video documentary) na kusikiliza kero na maoni ya wananchi kuhusu miradi ya kusambaza nishati bora vijijini.
Wananchi wengi waliofika katika banda la Wakala walitoa pongezi na shukrani kwa kupelekewa huduma ya umeme kupitia miradi ya kusambaza umeme vijijini. Hata hivyo, walijitokeza baadhi ya wananchi waliolalamikia baadhi ya vijiji vyao kutofikiwa na miundo mbinu ya umeme na kuomba maelezo ya mpango endelevu wa kusambaza umeme vijiji vyote Tanzania Bara.
Imeandaliwa na:
Jaina D. Msuya
Afisa Habari na Elimu kwa Umma
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mawasiliano Towers, Ghorofa ya 2
Barabara ya Sam Nujoma
S. L. P 7990
Dar es Salaam, Tanzania
Barua Pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 22 2412001, +255 22 2412002, +255 22 2412003
Nukushi: +255 22 2412007