Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kusambaza mitungi ya gesi 19,530 yenye thamani ya Shilingi milioni 390 katika wilaya sita za mkoa wa Mara ambapo mradi huo utawanufasiha wakazi wa maeneo ya vijijini.
Akizundua mradi huo leo, tarehe 21 Oktoba, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali, Evans Mtambi, Mkuu wa wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka amesema Serikali imeweka ruzuku kupunguza gharama ili Wananchi wajaribu matumizi ya nishati hiyo na kuona faida yake ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
Mhe. Chikoka amesema Mradi huo wa REA ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini huku Wananchi mkoani humo wakiiomba seijali kusogeza vituo vya kujaza gesi karibu na makazi yao.
Mitungi hiyo yenye ujazo wa kilo 6 kila moja itauzwa kwa bei ya ruzuku ili kuwezesha Wananchi wa maeneo hayo ya vijijini kuanza matumizi ya nishati hiyo na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yameelezwa kuwa na athari nyingi ikiwemo za kiafya na kimazingira.
Chikoka amesema mitungi hiyo inatarajiwa kusambazwa katika wilaya zote sita (6) za mkoa wa Mara na kueleza kuwa Serikali inatambua athari zinazowakumba Wananchi hasa Wanawake kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.
"Serikali inatambua changamoto zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa ukiachana na hili la mabadiliko ya tabia nchi lakini pia kuna suala la afya hivyo ikaona ipo haja ya kuja na mradi huu kwa maslahi mapana ya watu wake," amesema
Chikoka amewataka wakazi wa mkoa huo kutumia fursa hiyo ili kuweza kujipatia mitungi hiyo na kuanza safari ya matumizi ya nishati ya gesi katika mapishi yao ya kila siku.
Rais Samia Suluhu Hassan tayari alitangaza mkakati wa Serikali wa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini hadi kufika asilimia 80 mwaka 2034.
Chikoka amesema jamii inapaswa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia kwa maelezo kuwa mbali na faida za kiafya na mazingira pia matumizi ya nishati safi ni gharama nafuu ikilinganishwa na kuni na mkaa.
Akitoa taarifa ya mradi huo katika kijiji cha Etaro wilayani Musoma leo Oktoba 21,2025, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Geofrey Gedo amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti waathirika wengi wa matumizi ya nishati isiyokuwa salama ni Wanawake na Watoto jambo ambalo Serikali imeona ipo haja ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.
"Utafiti uliofanywa mwaka 2016 ulibainisha kuwa watu 33,024 hufarki nchini kila mwaka kabla ya wakati hii ni sawa na asilimia 8.49 ya vifo vyote nchini na vifo hivi hutokana na magonjwa ambayo yanachangiwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba huku waathirika wengi wakiwa ni Wanawake na Watoto," amesema.
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya kuni kama chanzo kikuu ca nishati ya kupikia nchini bado ni makubwa sana ambapo asilimia 63.5 ya kaya nchini zinatumia kuni kama chanzo cha nishati.
Amefafanua takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa matumizi ya mkaa ni asilimia 26.2 huku matumizi ya gesi iliyojazwa kwenye nitungi (LGP) ikiwa ni asilimia 5.1 pekee na umeme ukiwa unatumiwa kwa asilimia 3 huku vyanzo vingine vikiwa ni asilimia 2.2
Amesema kupitia mradi huo wa uuzwaji wa mitungi hiyo kwa bei ya ruzuku utasaidia kupandisha kiwango cha Watu wanaotumia nishati ya gesi nchini hivyo kuondokana na athari zinazotokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
"Mitungi hii itauzwa kwa bei ya ruzuku ambayo ni asilimia 50 ambapo kila mtungi pamoja na vifaa vyake utauzwa kwa Sh20,000 hii bei ni rafiki na tunaamini hata zile familia zenye kipato cha chini kitamudu," amesema
Wakizungumza kwenye uzinduzi huo baadhi ya wakazi wa kijiji cha Etaro wameiomba Serikali kuhakikisha nishati hiyo ya gesi inapatikana kwa ukaribu ili kuepuka gharama za ziada.
"Hapa kwetu angalau kuna sehemu gesi ikiisha unaweza kwenda kujaza kwasababu hapa senta kuna Wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hii lakini kuna maeneo mengi hakuna gesi hivyo ukihitaji inakubidi usafiri umbali mrefu," amesema Nyangeta Chimwejo.
Eva Willim amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi wananchi hasa wa vijijini hawana budi kuanza kutumia nishati ya gesi katika mapishi yao kwa maelezo kuwa upatikanaji wa miti na mkaa hivi sasa umekuwa wa shida.
"Zamani kuni zilikuwa zinapatikana kwa ukaribu zaidi lakini sasa hivi misitu yote imeteketezwa na matumizi ya binadamu, tunashukuru Serikali kutuletea mitungi hii kwani itakuwa ni hamasa kwa wengi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye gesi," amesema
Alex Kagere amesema usambazaji huo wa mitungi ya gesi maeneo ya vijijini ni mkombozi kwa wakazi wa vijijini hasa wanawake ambao wamekuwa wakitumia kuni wakati wa mapishi.
"Huu mradi ni mzuri kwasababu nyingi kwanza mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha nishati ya kuni kukosekana lakini madhara yanayotokana na mtumizi ya kuni pia ni mengi hivyo nitoe tu msisitizo Serikali iangalie namna ili gesi iwe inapatikana kwa ukaribu huku vijijini ili tukitaka kujaza tusipate shida," amesema
Amesema uharibifu wa mazingira pamoja na mambo mengine unasababishwa na matumizi ya nishati isiyo salama na ndio maana Rais Samia amekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwani ni faida kubwa kwa afya ya jamii na mazingira kwa ujumla.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la REA
28 Mtaa wa Medeli
Dodoma