Taasisi za Kifedha, Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo nchini,
wameshauriwa kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nishati hususani umeme
kushirikiana na serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ili kuongeza
kasi ya kuviunganisha vijiji vingi zaidi na umeme, ikiwemo kuwezesha mapinduzi
ya maendeleo kupitia nishati hiyo.
Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na
REA, kikijumuisha Taasisi za Kifedha, Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo,
Washirika katika tasnia ya nishati, na wawakilishi kutoka Wizara na Taasisi za
Serikali, kwa lengo la kujadili na kuangalia namna sekta hizo zinavyoweza
kushirikiana pamoja ili kuongeza nguvu ya kuhakikisha Tanzania hususan vijiji
vinaunganishwa na nishati ya umeme ili kuchochea shughuli za kiuchumi vijijini.
Akifungua kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
Mhandisi Ngosi Mwihava, alisema, miradi ya kuviunganisha vijiji na nishati ya
umeme ni eneo linalohitaji kuendelezwa kwa ushirikiano na wadau hao ili kuongeza
kasi ya uunganishaji umeme.
Alisema kuwa, tangu Wakala huo kuanzishwa mwaka 2007 kasi ya kuviunganisha
vijiji na umeme imeongezeka, na kuongeza kuwa, jitihada kubwa imekwishafanywa na
Serikali na endapo wadau hao wataunganisha nguvu, azma ya serikali kuhakikisha
kuwa ifikapo mwaka 2030 taifa zima liwe limeunganishwa na nishati hiyo
litafikiwa haraka kwa kuwa REA itakuwa na vyanzo vingi vya fedha.
Mwihava aliongeza kuwa, serikali imefanikiwa kuimarisha miundombinu ya
uzalishaji umeme jambo ambalo limewezesha kiwango cha uzalishaji kuongezaka
kutoka megawati 891 mwaka 2005 hadi 1,226.3, Machi 2015.
“Ikiwa vijiji vyetu vitaunganishwa na nishati hiyo, hali hiyo itachochea
shughuli za kiuchumi kufanyika ikiwemo kuanzishwa kwa viwanda vidogo katika
maeneo ya vijijini, na kuongeza huduma za kisasa za kiuchumi zinazotumia nishati
hiyo. Umeme ni maendeleo na ili tuendelee tunahitaji umeme,” alisema Mwihava.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Edmund Mkwawa, alieleza kuwa, endapo wadau
hao watashirikiana na REA, mradi huo utaleta matokeo makubwa zaidi ya
yaliyopatikana sasa na hivyo kuweza kuyafikia maeneo ambayo hayajafikiwa na
nishati hiyo. Aliongeza kuwa, zipo fursa nyingi ambazo taasisi hizo zinaweza
kuzitumia kupitia miradi mbalimbali ambayo itawezesha kupata faida na hivyo,
kikao hicho kitawawezesha wadau hao kutambua fursa hizo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa REA, Dkt. Lutengano Mwakahesya alitumia
fursa hiyo kuwashukuru wadau wote ambao wamewezesha Wakala huo kuunganisha miji,
vijiji na nishati hiyo kufikia asilimia 40 na kueleza kuwa, Wakala huo
utaendelea kutafuta wafadhili ili kuweza kufanikisha malengo yake ya kuhakikisha
kwamba taifa linaunganishwa na umeme.
Aliongeza kuwa, serikali peke yake haiwezi kufanya kazi hiyo na kueleza kuwa,
uhakika wa uwepo wa umeme utawezesha wananchi wengi zaidi kujiingiza katika
shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi anayeshughulikia nishati kutoka Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), Stella Mandago, alizitaka taasisi hizo kufanya kazi
na Wakala huo kwani zipo fursa nyingi na hivyo itawezesha taasisi hizo kupanua
wigo wa shughuli zao kiuchumi kupitia nishati ya umeme.
Na Asteria Muhozya
MEM News Bullettin Toleo No. 78