Waziri wa Nishati, Mh. Dk. Merdard Kalemani Aagiza Kuharakisha Utekelezaji wa Miradi ya Kusambaza Umeme Vijijini
Waziri wa Nishati Mh. Dk. Merdad Kalemani amewataka wadau wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza kushiriki kikamilifu na kuharakisha utekelezaji wake.
Dk. Kalemani alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa wadau hao uliofanyika tarehe 16 Julai, 2019 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam ambao ulijumuisha wakandarasi wanaojenga miundombinu ya kusambaza umeme vijijini, wazalishaji wa vifaa vya umeme, taasisi za fedha ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, benki za biashara, Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, Bodi ya Nishati Vijijini na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Katika mkutano huo ambao ulikuwa na lengo la kupanga mkakati bora wa kuharakisha utekelezaji wa mradi huo, Dk. Kalemani alisema wadau hawana budi kujipanga sawasawa ili watekeleze mradi kwa manufaa ya wananchi wa vijijini kwa kuwapatia huduma ya umeme ambayo itafanikisha lengo la ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuiwezesha nchi kuingia katika uchumi wa kati. “Huwezi kufikia lengo hilo bila nishati ya kutosha hivyo kila mtu achukue jukumu la kuharakisha kazi aliyopewa” alisisitiza.
“Kila mdau atimize wajibu wake, hatuna muda wa kutosha, tunataka Juni 2021 vijiji vyote vya Tanzania viwe vimefikishiwa umeme. Kila mtu achukue jukumu la kuharakisha kazi aliyopewa” alisisitiza na kuagiza Wakala wa Nishati Vijijini na Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) kuhakiki kazi za wakandarasi na kuhakikisha wanalipwa kwa wakati.
Aliomba mabenki na taasisi za kifedha kuweka masharti nafuu na kupunguza riba ili kampuni za Watanzania ziweze kumudu kukopa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme vijijini kwa haraka. Aidha, aliagiza wazalishaji wa vifaa vya kusambaza umeme vijijini kushusha bei ya vifaa hivyo na kutengeneza vifaa vyenye ubora. “Niyaombe mabenki na taasisi za kifedha yaingie jumla kuwezesha kampuni za Kitanzania kifedha ili watekeleze miradi ya Serikali wakiwemo wakandarasi wa umeme. Ukipewa kazi na Serikali unaaminika, mabenki yatoe fedha kwa kampuni za Kitanzania maana zimeaminiwa na Serikali” aliongeza Dk. Kalemani.
Naye Mwenyakiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo alisema Bodi yake imegundua kuwa kuna mlolongo mrefu wa malipo ambao unasababisha mkandarasi kutopata huduma ya vifaa kwa wakati na ndiyo sababu wamealika mabenki na taasisi za kifedha ili kwa kutumia utaalamu wao wa kifedha wasaidie kutatua tatizo hilo la ucheleweshaji wa malipo kwa watoa huduma za nguzo, transforma, nyaya za umeme na vifaa vinginevyo.
“Baada ya Bodi ya REA kukaa kikao na Wakandarasi na wauzaji wa vifaa vya kuunganisha umeme, na pia kuwatembelea wadau mbalimbali, tumegundua kuwa malipo toka REA hadi kumfikia mtoa huduma, ni mlolongo mrefu sana, ambao unafanya mkandarasi kutopata huduma ya vifaa kwa wakati muafaka, hadi LC zao zikamilike kuwa fedha kwenye akaunti za watoa huduma. Ndiyo maana tumeyaalika mabenki ili, kwa kutumia utaalamu wao wa kifedha, watusaidie kutatua tatizo la ucheleweshaji wa malipo kwa watoa huduma za nguzo, transforma, nyaya za umeme, na vinginevyo ambao mara nyingi hugoma kutoa huduma hiyo kutokana na hizi LC kuchelewa mpaka muda wake unapita bila kulipwa. Tunapenda Wakandarasi na watoa huduma tulizozitaja kukaa kwa pamoja, wajadiliane pamoja na REA ili tuone jinsi ya kufupisha mlolongo huu mrefu wa malipo” alisema.
Kwa upande wao wazalishaji wa vifaa vya umeme, wakandarasi pamoja na mabenki walilalamikia ucheleweshwaji wa malipo na kupendekeza Hati za Muamana zifuate taratibu za kimataifa.
Akifunga mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. Khamis Mwinyimvua aliwashukuru wadau kwa kushiriki katika mkutano huo na kuwaahidi kuwa maoni na mapendekezo yao yatazingatiwa na kuwataka wadau wote kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ili kuboresha ustawi wa jamii.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la LAPF, Ghorofa ya 7
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507