Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imeanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vipya vidogo vya gharama nafuu vya bidhaa za mafuta (petroli na dizeli) maeneo ya vijijini ili kuondosha madhara yatokanayo na njia zisizo salama. Madhara hayo ni pamoja na:
a) Gharama kubwa za upatikanaji wa bidhaa hizo maeneo ya vijijini tofauti na bei elekezi;
b) Gharama kubwa za usafiri hasa maeneo ya vijijini;
c) Kuadimika kwa bidhaa hizo maeneo ya vijijini;
d) Uuzaji na uhifadhi wa bidhaa za mafuta usio safi na salama (mapipa na madumu ya plastiki ndani ya nyumba);
e) Milipuko ya moto ambayo inaweza kugharimu maisha ya wananchi na hivyo kupunguza nguvu kazi ya Taifa;
f) Uharibifu wa mazingira unaotokana na bidhaa hizo kumwagika maeneo mbalimbali kwa sababu ya uhifadhi usiofaa;
g) Kuikosesha Serikali mapato ambayo wauzaji wa mafuta (petroli na dizeli) hawalipi kodi na tozo mbalimbali; na
h) Kuathiri afya kutokana na kuvuta hewa isiyo safi na salama kwa sababu ya kuhifadhi bidhaa hizo ndani ya nyumba.
Kwa kutambua hali hiyo, na kwa kuzingatia moja ya malengo ya Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015, ni wajibu wa Wakala kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa nishati na kwa bei nafuu katika maeneo yote ya nchi kwa njia iliyo salama.
Wakala wa Nishati Vijijini umetenga fedha kwa ajili ya kutoa mkopo nafuu kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kuuzia bidhaa za mafuta (petroli na dizeli) vijijini. Mkopo huu utasaidia uwezeshaji wa ujenzi na uendeshaji wa vituo vipya vidogo vya gharama nafuu maeneo ya vijijini ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya mafuta kwa gharama nafuu, kwa njia salama, na isiyo na madhara kwa mazingira.
Wakala unawasisitiza waombaji walioomba katika awamu ya kwanza na kutokidhi vigezo kuomba tena baada ya kufanya marekebisho ya mapungufu yaliyobainishwa katika maombi yao. Aidha maombi mapya ya mkopo yanakaribishwa.
Pamoja na tangazo hili, zimeambatanishwa nyaraka zifuatazo:
a) Fomu ya Maombi ya Mkopo wa Ujenzi wa Vituo Vidogo vya Mafuta Vijijini;
b) Mwongozo wa Utoaji Mkopo wa Ujenzi wa Vituo Vidogo vya Mafuta Vjijijini; na
c) Tangazo la Fursa ya Ujenzi wa Vituo Vidogo vya Mafuta Vijijini.
Utaratibu utakaotumika kutekeleza mradi huu umeainishwa katika mwongozo wa mradi ambao unapatikana kupitia tovuti ya Wakala ambayo ni www.rea.go.tz.
Mwongozo huo umeainisha vigezo vitakavyotumika kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuleta matokeo chanya yanayokusudiwa na Serikali. Mwongozo umeainisha namna ya kuomba mkopo, uidhinishwaji wa mkopo, vigezo vya mwombaji vya kiufundi na vya kifedha na masharti ya mkopo. Inasisitizwa waombaji kuzingatia matakwa ya mwongozo wakati wa kuwasilisha maombi ya mkopo.
Mwombaji atatakiwa kujaza fomu maalum ambayo inapatikana pia katika tovuti ya Wakala wa Nishati Vijijini (www.rea.go.tz). Maombi yaliyokamilika pamoja na viambatisho vyake yawasilishwe kwa njia ya zifuatazo:
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Barabara ya Medeli,
S. L. P. 2153,
DODOMA, TANZANIA.
Juu ya bahasha baada ya anuani ya Wakala iandikwe ‘Maombi ya Mkopo kwa Ajili ya Ujenzi wa Vituo vya Mafuta Vijijini’.
Pia mwombaji anaweza kuwasilisha maombi kupitia njia ya mtandao kwa barua pepe: vituovyamafuta@rea.go.tz.
Mwisho wa kuwasilisha maombi ni kama ifuatavyo:
a) Dirisha la maombi ya mkopo litafungwa pale ambapo idadi ya vituo 160 itakapofikiwa kulingana na bajeti iliyopo;
b) Ikumbukwe kuwa kila baada ya miezi mitatu tathmini itafanyika kwa maombi yatakayokuwa yamepokelewa;
c) Tathmini zitafanyika katika miezi ifuatavyo: 3,6,9 na wa 12; na
d) Tunawahimiza waombaji kuwasilisha maombi yao mapema iwezekanavyo ili waweze kunufaika na fursa hii.
Kwa maelezo zaidi kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijijini yawasilishwe kupitia barua pepe iliyotajwa hapo juu na kwa njia ya simu wasiliana na wafuatao:
Jina: Mha. Kelvin Tarimo
Namba ya Simu: 0713 230358
Jina: Mha. Ramadhani Mganga
Namba ya Simu: 0754 909237
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini
Jengo la Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Barabara ya Medeli
S. L. P. 2153
DODOMA, TANZANIA