TIMU ya mpira wa wavu ya wanawake ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), inayojulikana kama 'REA Queens', imeanza kwa kishindo michuano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) mwaka 2026 mkoani Morogoro.
Katika mchezo huo uliopigwa mkoani hapa, REA Queens walionyesha kiwango cha juu na kuwachapa bila huruma wapinzani wao, Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa jumla ya seti mbili bila majibu (2-0).
REA Queens ilitumia vyema makosa ya kiufundi yaliyofanywa na TRC na kufanikiwa kutawala seti ya kwanza kwa ushindi wa alama 25-13.
Baada ya mapumziko mafupi, warembo hao wa REA waliendeleza mashambulizi makali na ya mfululizo yaliyowachanganya kabisa wapinzani wao, ambapo walijihakikishia ushindi mwingine wa alama 25-14 katika seti ya pili.
Kufuatia pointi hizo, waamuzi walihitimisha mchezo huo kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, kwani TRC isingeweza kupindua matokeo baada ya kupoteza seti zote mbili za mwanzo.
Baada ya kuanza kwa rekodi hiyo nzuri, timu ya wavu ya REA inatarajiwa kushuka tena dimbani kesho, Novemba 11, 2026, kuikabili timu ngumu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pambano hilo la kukata na shoka linatarajiwa kupigwa katika viwanja vya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Bwaloni) mjini Morogoro.
-MWISHO-