Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar (MOWEM) imekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy yaliyolenga kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034).
Timu hiyo ambayo imeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Nishati wa MOWEM, Mhandisi Said Mdungi imekutana na Mkurugenzi Mkuu wa REA Novemba 10, 2026 katika Ofisi za REA Jijini Dodoma, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yao ya mafunzo na kubadilishana uzoefu.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Saidy ameihakikishia timu hiyo utayari wa Wakala kuendelea kutoa ushirikiano wakati wowote utakapohitajika ili kuwezesha utekelezaji wa Mkakati huo na kufikia malengo yaliyowekwa.
"Sisi tupo tayari na tuna hamu kubwa ya kushirikiana nanyi katika kutekeleza mpango huo," alisema Mhandisi Saidy.
Aidha Mhandisi Saidy amesisitiza umuhimu wa kuangalia namna ya kuwawezesha wananchi wenye uwezo mdogo wa kiuchumi kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha mabadiliko katika matumizi ya nishati hiyo yanawafikia wananchi wote bila kumuacha mtu nyuma.
Ameeleza kuwa pamoja na jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu kuweka mazingira yatakayowawezesha wananchi kumudu gharama za kuanza matumizi hayo.
"Unajua uzuri wa matumizi ya nishati safi, mwananchi akishaanza kutumia haachi, muhimu ni uhamasishaji ili mtu aanze kutumia," alisema Mhandisi Saidy.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Nishati wa MOWEM Mhandisi Said Mdungi ameishukuru REA kwa ushirikiano na utayari waliouonesha tangu siku ya kwanza ya ziara hiyo akieleza kuwa mafunzo na uzoefu walioupata umewapa mwanga kuhusu namna ya kuimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034).
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano na kubadilishana maarifa kati ya taasisi hizo kwa lengo la kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza upatikanaji na matumizi ya nishati hiyo nchini.