Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar (MOWEM), imetembelea Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034).
Timu hiyo iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Nishati MOWEM, Mhandisi Said Mdungi ilikutana na wataalam kutoka REA wakiongozwa na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage Novemba, 09, 2026 katika Ofisi za REA Jijini Dodoma.
“Tumeshuhudia REA mnafanya kazi nzuri nasi tumevutiwa kuja kujifunza hususan katika eneo hili la Nishati Safi ya Kupikia ili kufikia azma ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na uzoefu tutakaopata hapa utatusaidia utekelezaji,” alisema Mha. Mdungi
Akizungumzia uzoefu wa REA kwenye eneo hilo, Mha. Mwijage alieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Wakala ikiwemo uhamasishaji na uelimishaji wa wananchi kutambua athari za kutumia nishati isiyo salama pamoja na kuwafahamisha faida za kutumia nishati safi ya kupikia kufanikisha utekelezaji wa miradi ambayo utekelezwaji wake unaendelea huku akifafanua kila mradi kuanzia hatua ya mwanzo hadi utekelezaji unaoendelea hivi sasa.
“Katika kuhakikisha tunafikia lengo la Mkakati linalotutaka kuhakikisha 80% ya wananchi wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034, Wakala ulibuni miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa kusambaza majiko ya gesi ya kilo sita (LPG) kwa bei ya ruzuku ya 50% na huku tukilenga kila wilaya kupata majiko 3,255 na hadi sasa mradi huu umefikia zaidi ya 80% ya utekelezaji,” alifafanua Mha. Mwijage.
Mbali na mradi huo, Mha. Mwijage alielezea mradi wa usambazaji wa majiko banifu huku akielezea ufanisi wake na namna ambavyo mradi huo unatekelezwa kote nchini ambapo alisema awamu ya kwanza inayoendelea inahusisha usambazaji wa majiko banifu 200,000.
Kikao hicho ambacho kimefanyika katika ofisi za REA Jijini Dodoma, kimejadili uzoefu wa REA katika uanzishaji na uendelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia, pamoja na namna ya kushirikisha sekta binafsi katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Tunawezesha wazalishaji wa bidhaa na teknolojia za nishati safi ya kupikia na pia tutawezesha vikundi vya vijana na akina mama ili kuzalisha mkaa mbadala,” alifafanua Mha. Mwijage.
Miradi mengine iliyojadiliwa ni pamoja na mradi wa kuzalisha mkaa mbadala kwa kushirikiana na STAMICO, mradi wa kusambaza Gesi Asilia kwa kushirikiana na TPDC ambapo hadi sasa Kaya zipatazo 1,001 zimeunganishwa na awamu ya pili ya mradi ipo mbioni kuanza, na namna ambavyo REA ilivyowezesha Magereza yote nchini kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Katika mazungumzo hayo, wataalam wa REA wamepata fursa ya kueleza hatua zilizofikiwa, changamoto zilizojitokeza na mikakati inayotumika kukabiliana nazo.
Ziara hiyo ni sehemu ya kubadilishana uzoefu na maarifa yatakayosaidia kuimarisha juhudi za kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika sekta hiyo.