KASI ya kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika nchini imezidi kushika kasi, baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, kutoa jumla ya shilingi bilioni 10.78 kwa ajili ya kufanikisha mradi mkubwa wa uzalishaji wa nishati ya umeme jua kupitia mradi wa Bugando Solar Power, wilayani Magu mkoani Mwanza.
Mradi huo wa kimkakati wenye uwezo wa kuzalisha Megawati tano (5MW), sasa umeanza rasmi kuchangia nguvu katika Gridi ya Taifa, tangu ulipowashwa rasmi Septemba 23, mwaka huu, na kuleta matumaini mapya ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa mkoa huo na nchi nzima kwa ujumla.
Akizungumzia uwekezaji huo, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, alisema kati ya fedha hizo, shilingi milioni 561 zilitolewa mapema kama ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina, kutengeneza michoro, na kupanga paneli za jua ili kuhakikisha mradi unaleta tija.
Mhandisi Mwijage alibainisha kuwa mradi huo unatekelezwa kupitia ushirikiano wa pande tatu unaohusisha REA, Benki ya CRDB inayopitisha mikopo, na mwekezaji binafsi ambaye ni kampuni ya Bugando Natural Energy Ltd.
"Katika muundo wa gharama za mradi huu wenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 17.5, REA imechangia asilimia 61, Benki ya CRDB asilimia 11, na mwekezaji amechangia asilimia 27. Kupitia CRDB, mwekezaji amewezeshwa kupata mkopo wa shilingi bilioni 10.2 utakaolipwa kwa miaka 11, ukiwa na mwaka mmoja wa matazamio (grace period) ambapo atalipa msingi wa mkopo pekee bila riba," alisema Mhandisi Mwijage.
Alitaja manufaa makubwa ya mradi huo kuwa ni pamoja na kuongeza kiasi cha umeme kwenye gridi ya taifa, kuimarisha nishati maeneo yaliyokuwa na umeme mdogo, kulinda mazingira kwa kutozalisha hewa ukaa, na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi za ajira viwandani. Tofauti na zamani ambapo miradi kama hiyo ilinufaisha watu wachache wa karibu, sasa umeme wote unaingizwa kwenye mfumo wa kitaifa ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bugando Natural Energy Ltd, Bwana Joseph Jirabi, alisema kuwaka kwa mradi huo kumesaidia kutatua changamoto sugu ya uhaba wa maji wilayani Magu, iliyokuwa inasababishwa na ukosefu wa umeme wa kuendeshea mitambo ya kusukuma maji.
"Baada ya kuwashwa kwa chanzo hiki mnamo Septemba 23, hali imeanza kuimarika na wananchi sasa wanashuhudia mabadiliko chanya katika uendeshaji wa mashine za kusukuma maji na kuongeza upatikanaji wa maji safi majumbani mwao," alisema Bwana Jirabi huku akiishukuru serikali kupitia REA kwa msaada wa kisera na kifedha.
Kufuatia mafanikio hayo, REA imetoa wito kwa waendelezaji wengine wa miradi ya nishati jadidifu kujitokeza na kuchangamkia fursa hizo za uwekezaji, ikiahidi kuwa milango ipo wazi kuwasaidia kuandaa nyaraka sahihi na thabiti ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya kibiashara.