Mwanza ๐
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) uko katika hatua za mwisho kukamilisha mradi mkubwa wa ufungaji wa taa 214 za barabarani katika Chuo Kikuu cha St. Augustine cha Tanzania (SAUT); Jijini Mwanza, hatua itakayoboresha mazingira ya usalama na kujifunzia kwa wanafunzi 13,600. Mradi huo unaoangazia barabara na maeneo ya chuo kwa urefu wa kilomita 6.42, unalenga kujenga mazingira rafiki na yenye ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo yao kwa urahisi wawapo chuo hapo, hususan nyakati za jioni na usiku.
Mageuzi haya ya miundombinu si tu kwamba yanatafsiri dhamira ya REA katika kuleta nishati ya kimkakati, bali pia yanapanua fursa za kitaaluma na kuimarisha ulinzi ndani ya taasisi hiyo kubwa ya elimu ya juu nchini.
Mradi huu umegharimu jumla ya shilingi milioni 826.6, ambapo Serikali kupitia REA imechangia shilingi milioni 793.8 na chuo chenyewe kimechangia shilingi milioni 32.8 Hatua hii ni sehemu ya mikakati endelevu ya kuleta nishati safi na salama katika taasisi za elimu ili kuinua kiwango cha taaluma nchini.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi, Advera Mwijage, tarehe 15 Oktoba, 2026 Chuo hapo baada ya kutembelea na kujionea maendeleo ya Mradi huo alieleza kuwa (REA) ina programu mbalimbali za kusambaza umeme vijijini; kuwezesha sekta binafsi kuzalisha umeme; kukuza nishati safi ya kupikia, na kuwezesha upatikanaji wa taa kwenye taasisi zinazohudumia jamii kubwa ya watu kama vyuo vikuu.
"Katika chuo hiki cha SAUT, tumefunga taa 214 kwenye mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 6.42. Tumeshuhudia uhitaji mkubwa sana hapa kwa sababu hapo awali, wanafunzi walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama wakati wakielekea mabwenini nyakati za usiku, ikiwemo kuvamiwa, kupokwa kompyuta mpakato (laptop) na simu zao," alisema Mhandisi, Advera.
Aliongeza kuwa kuwekwa kwa mfumo huo wa taa za sola kutawawezesha wanafunzi zaidi ya 13,600 kusoma na kuishi katika mazingira rafiki, salama na yenye ubora wa hali ya juu, Aidha, alitoa wito kwa Halmashauri zilizonufaika kwa miradi ya taa na kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha SAUT kuhakikisha ulinzi na matengenezo ya miundombinu hiyo, ikiwa ni pamoja na kuzisafisha taa hizo nyakati za vumbi na kuzikarabati haraka changamoto zinapojitokeza.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Sr. Clara Rupia ameupokea mradi huo kwa furaha kubwa, akibainisha kuwa umeme huo unakwenda kubadilisha maisha ya kila siku ya wanafunzi na watumishi. Alieleza kuwa chuo hicho huendesha masomo kuanzia asubuhi saa 1:00 hadi usiku saa 2:30 au saa 3:00 kasoro, hivyo mwanga huo utawasaidia sana wanafunzi kutembea kwa usalama katika maeneo ya madarasa na mabwenini.
"Kwa niaba ya jumuiya ya SAUTI, tunaishukuru sana serikali. Hapa chuoni ni kitovu cha malezi ambapo tunawaandaa Watanzania watakaokwenda kulitumikia taifa la kesho na keshokutwa, ili tufikie Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050," alisema Profesa Sr. Clara.
Naye Msimamizi wa ufundi wa mradi huo; Fr. Cletus Uhinga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha, Chuo Kikuu cha SAUTI alisema kuwa hadi sasa takriban asilimia 60 hadi 65 ya taa hizo zimeshafungwa na kuanza kutumika (Kuwashwa). Aliongeza kuwa mwanga huo ni mkubwa kiasi kwamba baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitumia fursa hiyo kukaa chini ya taa hizo nyakati za usiku kwa ajili ya kujisomea.
“Jamii ya chuo cha SAUTI imetoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Bodi na Uongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kufanikisha mradi huo uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu baada ya kukosa ufadhili mara kadhaa kutoka kwa wafadhili wengine hapo awali.” Amesema Fr. Cletus.
- MWISHO –