Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Sengerema iliyopo mkoani Mwanza imefanikiwa kupunguza gharama za nishati ya kupikia kwa zaidi ya asilimia 50. Hii ni baada ya kufikiwa na mradi wa nishati safi ya kupikia, unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Shule hiyo yenye tahasusi za kidato cha tano na sita ina jumla ya wanafunzi 1,422, ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya matumizi ya kuni. Hali hiyo ilikuwa ikisababisha uharibifu wa mazingira pamoja na kuchelewa kwa ratiba za chakula cha wanafunzi kutokana na changamoto za upatikanaji wa kuni wakati wa vipindi vya mvua.
Akizungumza wakati wa mahojiano maalum, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavualana ya Sengerema, Bwana Zakaria Kahema halibainisha kuwa hapo awali walikuwa wakitumia wastani wa shilingi milioni 6 hadi milioni 7 kwa mwezi kwa ajili ya ununuzi wa kuni pekee. Hata hivyo, baada ya kufungiwa mifumo hiyo mipya na kupokea tani 22.3 za mkaa mbadala, gharama hizo zimeshuka hadi kufikia shilingi milioni 3 hadi milioni 3.5 kwa mwezi.
"Hali ilikuwa ngumu sana kipindi tunatumia kuni, hasa kukiwa na mvua. Ratiba za darasani zilikuwa zikiathirika kwa sababu wanafunzi walikuwa wakichelewa kupata chakula. Lakini sasa hivi, tunashukuru sana mifumo hii mipya imebadilisha kabisa mazingira yetu ya kazi, hakuna moshi na chakula kinawahi kwa wakati," alisema mmoja wa wapishi wa shule hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA. Mhandisi Advera Mwijage amesema kuwa mradi huo uliogharimu shilingi milioni 47.6 umejumuisha usambazaji wa majiko makubwa 11 ya kisasa; sufuria zake pamoja na tani 20 za kuni mbadala (Kuni poa). Shule ya Sengerema ni miongoni mwa shule kongwe zilizopewa kipaumbele katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa agizo la serikali lililotolewa Machi 24, 2023, linalopiga marufuku matumizi ya kuni kwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100.
Mhandisi Advera, ametoa wito kwa uongozi wa shule hiyo na taasisi nyingine zilizofikiwa na mradi huo kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuleta tija iliyokusudiwa na serikali katika kulinda afya za wapishi na kuhifadhi misitu na kutunza mazingira.