Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umekusudia kuanzia mwaka 2024 kufikisha miundombinu ya umeme hadi kwenye vitongoji baada ya kukamilisha utekelezwaji wa mradi wa kuunganisha huduma hiyo kwenye vijiji vyote nchini.
Imeelezwa kuwa, hadi sasa usambazaji wa umeme vijijini umefikia asilimia 80 tangu kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili mwezi Julai 2018 wa kufikisha umeme vijijini. Ni Vijiji 758 tu vilivyobaki kati ya Vijiji 12,315 vilivyopo nchi nzima; na wakandarasi wote waliopewa zabuni wamefikia asilimia 75. Ifikapo mwisho wa mwezi Februari 2024 wakandarasi wote watakuwa wamekamilisha utekelezaji wa miradi yao.
Akizungumza hivi karibu mkoani Pwani baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo na kufanya tathimini ya mwaka mzima wa utekelezaji mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Thomas Mmbaga alisema kuanzia mwaka huu 2024, Wakala utakuwa unapeleka umeme katika ngazi ya vitongoji.
“Mkakati unakuja, baada ya miundombinu kufikishwa katika kila makao makuu ya kijiji, vijiji vingi ni vikubwa na vina vitongoji kuanzia vitano na kuendelea; mkakati wa kufikisha umeme katika vitongoji vyote utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha”, alisema.
Alisema baada ya kukamilisha vijiji 758 vilivyofikiwa na huduma ya umeme, watapeleka miundombinu hiyo katika jumla ya vitongoji 3,060.
Awali, Katika ukaguzi huo Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati ya Umeme Vijijini (REB); Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu alisema ameridhishwa na namna taasisi hiyo inavyosimamia utekelezwaji wa mradi huo.
“Nimeona mafanikio makubwa katika Wilaya tatu za mkoa wa Pwani nilizotembelea nikianza na Mkuranga, Kisarawe, Kibiti na Rufiji. Huduma imefika zaidi ya asilimia 90; bado vijiji vichache havijafikiwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuzungukwa na maeneo oevu yenye majimaji”, alisema Balozi Kingu.
Alisema kwa vijiji vilivyofikiwa na huduma hiyo, ni muhimu kwa Wananchi kuanza kuchangamkia kutumia fursa ili iwe kichocheo na chachu katika kukuza shughuli zao za kiuchumi.
"Kama Mwenyekiti wa Bodi nitahakikisha natoa uongozi kwa REA kuona ndoto zetu zinafikiwa za kufikisha huduma ya umeme vijiji vyote nchini katika kutimiza azma ya serikali", alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini alisema bado ataendelea kufanya ziara za mara kwa mara kukagua maendeleo ya utekelezwaji wa miradi katika mikoa mbalimbali lengo likiwa kuhakikisha shughuli hiyo inakamilika ifikapo Juni 2024.
Mkurugenzi Mkuu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Jengo la PSSSF, Ghorofa ya 7
Barabara ya Makole
S. L. P 2153
Dodoma, Tanzania
Barua pepe: info@rea.go.tz
Simu: +255 262323504, +255 262323506, +255 262323507